Na Oscar Assenga,Tanga
kuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupimwa kwa kiwango cha uwekezaji au ujenzi wa viwanda pekee, bali kwa namna serikali na jamii zinavyoweka fursa za usawa wa kijinsia katika ajira, hususan kwa watoto wa kike na wa kiume.
Dk Burian ameyasema hayo alipokuwa akifungua maadhimisho ya nne ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Sekta ya Bahari yaliyofanyika jijini Tanga (Jumapili) Mei 18/2025.
Akimnukuu mwanafalsafa maarufu Plato, aliyewahi kusema kuwa “Kilimo cha jamii yoyote ni jinsi inavyowathamini wanawake”, Dk Burian alisisitiza kuwa taifa linapaswa kujipangia malengo ya kuhakikisha usawa wa kijinsia unatekelezwa kikamilifu.
“Tusiache mwanamke abaki ufukweni bali tunataka aingie ndani ya bahari,” alisema kwa msisitizo..
Alieleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, sekta ya bahari bado inatawaliwa na wanaume, huku takwimu zikionyesha kuwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta hiyo ni asilimia 1.2 pekee.
Katika hatua ya kutia moyo, Dk Burian alipongeza Umoja wa Wanawake Wanaofanya Kazi katika Sekta ya Bahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) kwa kuanzisha programu ya ‘Wakamate Wangali Wadogo’ (Catch them Young) inayolenga kuelimisha na kuwahamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na fani zinazohusiana na bahari.
Alisisitiza kuwa wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta hiyo, akibainisha kuwa juhudi kama hizo zinaunga mkono maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye elimu ya sayansi kwa watoto wa kike, ikiwemo kuanzishwa kwa shule maalum.”
Hapa Tanga, kupitia uwekezaji wa Rais, tumeanzisha shule maalum ya watoto wa kike wilayani Kilindi ambayo imepewa jina la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Beatrice Shelukindo,” alisema.
Dk Burian pia alitoa wito kwa sekta binafsi inayohusika na bahari kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika ajira.
“Nifahari yetu Kuwaona Wanawake wa Kitanzania wakiongoza na kushiriki miradi mkubwa ya maendeleo ya bandarini,fukwe zetu wakifundisha kwenye vyuo vya Bahari kama Chuo Cha Bahari Dar es salaam(Dar es salaam Maritime INstute-DMI)kufanya kazi kwenye Meli za kitaifa na Kimataifa Kwa hakika Hawa ni vinara na fahari yetu ni lazima tuwapongeze”alisema Burian.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA, Bi Fortunata Kikwaya, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika sekta ya bahari.”
Sherehe hizi za nne zinaashiria maono yetu kuwa wanawake si wa kushirikishwa tu, bali ni wadau wakuu katika maendeleo ya sekta hii,” alisema.
Bi Kikwaya alitaja mafanikio ya WOMESA kuwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka 24 mwaka 2021 hadi kufikia 174 mwaka huu, pamoja na kudhamini mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wanawake.
Kuhusu mpango wa ‘Catch them Young’, alisema tayari wametembelea shule 35 na kuanzisha vilabu tisa vya wanafunzi, vitatu kati yake vikiwa jijini Tanga.
Hata hivyo, alieleza kuwepo kwa mwamko mdogo wa wanawake kujiunga na WOMESA pamoja na uelewa mdogo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bahari.
Aliiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaotaka kusomea taaluma zinazohusiana na sekta ya bahari na kusaidia kuendeleza juhudi za kuwahamasisha kuingia katika sekta hiyo.