Mwandishi Wetu, Singida
MAELFU ya wakulima wilayani Iramba wameanza kunufaika na mbinu za kilimo chenye tija kupitia mradi wa NOURISH unaotekelezwa na mashirika ya SNV na Farm Africa kwa ushirikiano na RECODA na MIICO.
Kupitia maadhimisho ya Siku ya Wakulima wa NOURISH, wakulima wamepatiwa elimu ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, lishe bora na usafi wa mazingira.
Akizungumza katika kijiji cha Ngalagala, Afisa Mradi huo, Salome James ameeleza kuwa mradi huo unasaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na miundombinu duni.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, zaidi ya bustani 310 za mbogamboga zimeanzishwa, vikundi 59 vya wakulima vimeundwa na mashamba darasa 174 yameanzishwa.
Amesema mbegu na viazi lishe vimesambazwa, huku wakulima 320 wakifanyiwa upimaji wa afya ya udongo ili kuongeza tija shambani.
Kwa upande wake, Ofisa Tarafa, Charles Makala, aliwahimiza wakulima kutumia kikamilifu teknolojia na maarifa waliyopewa kwa maendeleo ya jamii zao.
Mradi wa NOURISH unaolenga wakulima wadogo na biashara ndogo katika mikoa mitano nchini, unafadhiliwa na Norad na unatekelezwa kwa miaka mitano (2024–2028) ili kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu wa tabianchi.