Na WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amewasihi wanafunzi 120 kutoka wilayani humo wanaoelekea kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa kwa mwaka 2025, kuzingatia nidhamu, maadili na juhudi ili kufanikisha ushindi katika mashindano hayo.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa kuwaaga wanamichezo hao ambapo Kasilda aliwatakia safari njema na mafanikio mema, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua dhamana waliyopewa na wilaya yao.
“Nendeni mkashindane kwa bidii na kuhakikisha mnaleta vikombe kwa michezo mliyofundishwa aidha zingatieni nidhamu ya hali ya juu na jiepusheni na tabia hatarishi zinazoweza kuathiri maisha yenu na jamii kwa ujumla,” alieleza Kasilda.
Aidha, alibainisha kuwa mafanikio ya wanamichezo hao katika mashindano ya mkoa yatasaidia kuwatoa wachezaji wengi zaidi kutoka wilaya ya Same watakaowakilisha mkoa ngazi ya Taifa.
Hata hivyo, Kasilda aliwashukuru wadau ambao kwa namna ya pekee walijitolea kwa hali na mali kudhamini michezo hiyo ya UMITASHUMTA kwa mwaka 2025 huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ili kukuza vipaji.
Mashindano ya UMITASHUMTA hufanyika kila mwaka yakilenga kuibua vipaji na kukuza michezo miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi nchini.