Na Jane Edward, Arusha
Maandalizi ya Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii (KILIFAIR 2025) yanaendelea kwa kasi, huku tukio hilo kubwa likitarajiwa kufanyika kwa mafanikio makubwa katika jiji la Arusha. Maonyesho haya, ambayo hufanyika kila mwaka, yamejizolea sifa kama jukwaa muhimu la kukuza biashara za utalii, kuunganisha wadau wa sekta hiyo, na kutangaza vivutio vya kipekee vya Afrika kwa ulimwengu mzima.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hilo, zaidi ya wanunuzi na mawakala wa usafiri 780 kutoka mataifa mbalimbali duniani tayari wamethibitisha ushiriki wao katika KILIFAIR 2025. Aidha, zaidi ya wageni 15,000 kutoka nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kushiriki, ishara ya ukuaji wa sekta ya utalii wa kikanda na umaarufu wa KILIFAIR kama jukwaa la kimataifa.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkurugenzi wa KILIFAIR, Bw. Dominick Shoo, amesema:
“Tumejipanga kwa hali ya juu kuhakikisha KILIFAIR 2025 inakuwa ya kipekee zaidi. Ushiriki wa wadau kutoka zaidi ya nchi 14 ni uthibitisho kuwa Arusha imekuwa kitovu cha utalii Afrika Mashariki. Tunatarajia kuona ushirikiano mpya, ubunifu na mikataba ya kibiashara inayochochea maendeleo ya sekta yetu.”
Ujenzi wa mabanda ya maonyesho unatarajiwa kuanza rasmi Jumapili, ambapo maandalizi ya mwisho yataanza kuwekwa tayari kwa ajili ya siku kadhaa za tukio hilo. Mabanda hayo yatatumika na kampuni binafsi, taasisi za serikali na washirika wa maendeleo kuonyesha huduma, bidhaa na vivutio vyao vya utalii.
Mataifa yatakayoshiriki kwa mwaka huu ni pamoja na Ujerumani, Uganda, Uturuki, Afrika Kusini, Zanzibar, Zambia, Ethiopia, na Rwanda – yote yakileta wawakilishi wa sekta ya utalii, biashara na uwekezaji.
Kipengele kipya kwa mwaka huu ni uzinduzi wa “East Africa Pavilion”, eneo maalum linalokusanya nchi za Afrika Mashariki kuonyesha vivutio vyao kwa pamoja. Jukwaa hili lina lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza mwonekano wa Afrika Mashariki katika ramani ya utalii wa kimataifa.
KILIFAIR 2024 inatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya utalii barani Afrika, ikileta pamoja washirika wa maendeleo, wawekezaji, watoa huduma na wanunuzi kutoka pande zote za dunia
Mwisho..