NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Shirika la Viwango Barani Afrika (ARSO) utakaofanyika kuanzia Juni 23 hadi 27, 2025, katika visiwa vya Zanzibar, ambapo Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza leo Mei 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema mkutano huo unatarajiwa kuwahusisha takribani wageni 300 kutoka zaidi ya nchi 50, wakiwemo wanachama wa ARSO na wadau wa viwango kutoka ndani na nje ya Afrika.
Dkt. Katunzi amesema kuwa tukio hili litakuwa fursa ya kipekee kwa Tanzania kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, hususan kwa wazalishaji wanaotafuta masoko ya nje ya nchi.
“Ni fursa kwa wazalishaji wetu kupata masoko ya nje ya nchi ili kukuza biashara na kuendelea kuchangia uchumi endelevu wa taifa letu,” amesema Dkt. Katunzi.
Amesisitiza kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa kimataifa ni uthibitisho wa kuimarika kwa ushiriki wa Tanzania katika masuala ya uandaaji wa viwango na udhibiti wa ubora barani Afrika.
Aidha, mkutano huo utaambatana na maonesho ya biashara, na Dkt. Katunzi ametoa wito kwa wazalishaji na watoa huduma wa ndani, ikiwemo sekta ya utalii, kujitokeza kushiriki na kudhamini, ili kutangaza bidhaa na huduma zao kwa wageni wa kimataifa.
Kauli mbiu ya mkutano huu ni: “Kuharakisha haki katika biashara ndani ya eneo la biashara huria barani Afrika (AfCFTA) kupitia mifumo madhubuti na viwango vilivyooanishwa.”