Na Seif Mangwangi, Arusha.
WADAU wa asasi za kiraia nchini wametakiwa kutumia wiki ya AZAKI 2025 iliyoanza leo Jijini Arusha kutathmini changamoto zinazowakabili na kuja na suluhu itakayosaidia asasi hizo kuwa endelevu kwa maendeleo ya watanzania.
Wito huo umetolewa leo Juni 2, 2025 na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Foundation for Civil Society (FCS), CPA, Merci Silla katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa wiki ya AZAKI 2025 jijini hapa.
Amesema katika siku za hivi karibuni mashirika ya kijamii (Azaki), yamekuwa yakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha jambo ambalo limekuwa likihatarisha uendelevu wake.
” kazi mojawapo ya Azaki ni kusaidia serikali kutoa huduma shirikishi na kuleta maendeleo kwa wananachi wake, ni wazi tunatakiwa kutafakari changamoto zinazotukabili ili kuzipatia suluhu na mwisho tuweze kufanyakazi hii ya kuisaidia serikali,” Amesema.
Amesema ni wakati wa asasj za kiraia kujenga mshikamano na kusonga mbele, kuangazia fursa mpya za kujenga mshikamano huo ili kupata maendeleo ya pamoja.
Mkurugenzi wa Vodacom Foundation Zuwein Farah amesema tangu kulipoanzishwa wiki ya azaki nchini wamekuwa wakijitahidi kuwa moja ya wafadhili wakuu lengo likiwa ni kuonyesha mchango wa taasisi hiyo kwa jamii.
” Vodacom Tanzania tunajivua kuwa moja ya wafadhili wakuu wa wiki ya Azaki nchini, kupitia Vodacom Foundation tumekuwa tukifadhili miradi mingi katika sekta za Afya, Elimu, michezo, mazingira lengo kuu likiwa ni kumsaidia Mtanzania,” amesema.
Mkuu wa kitengo cha wateja katika benki ya Stanbic, Doreen Dominick ambaye ni mmoja wa wadhamini na washiriki wiki ya azaki 2025 amesema kauli mbiu ya wiki ya azaki mwaka huu ya ” Nyenzo ya maendeleo(path to progress” inaakisi maendeleo ya kweli ambayo watanzania wanapaswa kuyapata kupitia msaada wa azaki.
Amesema Stanbic imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo nchini ambapo imeweza kuwajengea uwezo na kuwawezesha mikopo mbalimbali na kuwatafutia masoko wajasiriamali 6500 ambao kati yao wanawake ni asilimia 65.