Na Mwandishi Wetu,Songea
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele iliyofanyika nyumbani kwa marehemu eneo la Mahenge, mjini Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika shughuli hiyo, Dkt. Nchimbi amemuelezea Hayati Songambele kama mmoja wa mashujaa waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa Tanzania na kujenga misingi ya taifa jipya baada ya ukoloni.
Dk.Nchimbi amesema Hayati Songambele alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha TANU na alishiriki kikamilifu katika harakati za kujenga taifa huru na lenye mshikamano.
“Tuendelee kujifunza kutoka kwa wazee hawa ambao wamefariki wakiona amani na upendo wa Tanzania ukiendelea, heshima pekee tunayoweza kuwapa ni kuendeleza mshikamano, amani na maendeleo ya nchi yetu…
“Tuendelee kujua sisi ni Taifa moja, tuna wajibu wa kupendana na kujiepusha na vishawishi vyote ambavyo vinaweza vikavuruga amani na kuvunja mtangamano wa kitaifa,” alisema Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa sana na msiba huo, akimwelezea Hayati Songambele kama kiongozi mwenye moyo wa kipekee wa kulitumikia taifa kwa hali na mali, na kwamba wananchi wa Ruvuma wana kila sababu ya kujivunia mchango wake mkubwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kifo cha Mzee Songambele ni pigo kubwa kwa Taifa, akieleza kuwa marehemu alikuwa ni hazina ya busara na kumbukumbu muhimu ya historia ya Tanzania.
“Hakuwa tu kiongozi bali alikuwa taa na mwelekeo katika giza la ukoloni, aliyesimama kidete kwa ujasiri, hekima, na moyo wa kizalendo katika kuijenga Tanzania mpya. Alisimama kwa haki, kupitia juhudi zake na viongozi wenzake wa wakati huo, tunauona leo mwanga wa uhuru, umoja, na amani uliodumu kwa zaidi ya nusu karne,” alisema Kanali Ahmed.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Mtoto wa Hayati Songambele, Rajab Songambele amesema wataendelea kuyaenzi na kuyatekeleza mema yote waliyofundishwa na Mzee wao ili yadumu kwa vizazi vijavyo.
Hayati Alhaj Mustafa Mohamed Songambele alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa Chama cha TANU akiwa miongoni mwa wanachama wa kwanza 30 wa chama hicho, na alipata kadi ya uanachama namba 27.
Alizaliwa Mei 25, 1925 katika eneo la Bombambili, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma na amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100.