Na Pamela MollelArusha.
Kampuni ya Bima Zanzibar (ZIC) imewataka wageni wanaotembelea katika kisiwa hicho kuhakikisha wanakata bima ya usafiri kwa ajili ya kujiwekea ulinzi kwa dharura yoyote inayoweza kujitokeza katika utalii wao.
ZIC imeyasema hayo ndani ya viwanja vya Kisongo vilivyoko Mkoani Arusha kwenye maonyesho makubwa ya kimataifa ya Karibu-Kili Fair yaliyoanza june 6-8, 2025.
Maonyesha hayo ya Afrika Mashariki yamekutanisha waonyeshaji, mawakala na wawekezaji wa utalii zaidi ya 500 kutoka nchi 40 duniani.
Meneja masoko kutoka shirika la bima la Zanzibar(ZIC), Mohammad Said Matumula amesema kuwa wameshiriki katika maonyesho hayo ili kutoa elimu kwa wadau wa utalii juu ya huduma wanazozitoa.
“Tumekuja kuwaonyesha huduma tunazotoa ambazo mbali na kuwa suluhu ya changamoto lakini pia zina manufaa dhidi ya shughuli na maisha yao kwa ujumla” amesema Matumula.
Akizungumzia moja ya bidhaa wanazotoa kwa wadau wa utalii, Matumula amesema kuwa ni bima ya usafiri ‘In bound Travel Insurance’ yenye lengo la kuboresha ulinzi kwa watalii wote wanaoingia ndani ya visiwa vya Zanzibar.
“Bima hii itampa mgeni huduma ya changamoto yoyote ya dharura itakayojitokeza ikiwemo Matibabu kwa watakaopata ajali wakiwa katika maeneo ya vivutio vya utalii, huduma za Uokoaji, Fidia ya kuchelewa au kupotea kwa mizigo na Msaada endapo mgeni atapoteza hati ya kusafiria”amesema Matumula.
Awali akifungua maonyesho hayo, Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko aliwataka wizara ya maliasili na Utalii kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii nchini lakini pia kutumia ukuaji wa sekta ya Tehama kutangaza utalii wa Nchi.
Pia amewataka sekta binafsi kuendelea kushirikiana na serikali kuinua sekta ya utalii ikiwemo kuongeza uwekezaji na utangazaji wa utalii nchini ili kuongeza pato la Taifa.
“Sisi kama serikali tutaendelea kuondoa vikwazo vyote kwenye uwekezaji wa sekta hii muhimu nchini ili wananchi wetu wanufaike nao kiuchumi”amesema.
Mkurugenzi wa Karibu-Kili fair, Dominic Shoo amesema kuwa zaidi ya makampuni na mawakala 500 zimeshiriki kutoka nchi 40 duniani kuja kuonesha huduma zao, kujionea vivutio vilivyoko nchini lakini pia kufanya biashara na wawekezaji na watoa huduma za utalii nchini.
“Kubwa ni kuutangaza utalii wetu katika mataifa makubwa duniani, kuja kujionea tulivyonavyo, waje watuoneshe wanavyofanya lakini pia wavutiwe na fursa za uwekezaji zilizoko nchini” amesema.
Amesema katika maonyesho hayo zaidi ya watu 15,000 wanatarajia kuhudhuria kwa siku tatu lakini ndani yake mafunzo na biashara vitatawala.