Mkuu wa Chuo Cha Mafunzo Ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa mafunzo ya kwanza ya kiraia ya ulinzi wa amani nchini. Washiriki 22 wanatarajiwa kushiriki mafunzo hayo yaliyoanza leo Juni 9 2025 na yanatarajiwa kumalizika Juni 13, 2025.
TANZANIA imezindua mafunzo ya kwanza ya kiraia ya ulinzi wa amani kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha amani endelevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam leo Juni, 2025 Kamanda wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mfumo wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa unaojumuisha vipengele vitatu vikuu vya kiraia, polisi na jeshi.
Amesema kuwa mafunzo hayo, yanayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia UNDP, yanasimamiwa na Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) na yanalenga kuwajengea washiriki ujuzi na maarifa yanayohitajika katika kuendeleza amani ya kudumu, utatuzi wa migogoro na ujenzi wa jamii baada ya migogoro katika ukanda huu.
“Hili ni tukio muhimu linaloashiria hatua kubwa katika kuimarisha uwezo wa kikanda na kitaasisi katika ujenzi wa amani, kukabiliana na migogoro, na shughuli za ujenzi wa jamii baada ya migogoro,” amesema Brigedia Itang’are.
Amebainisha kuwa mienendo ya migogoro katika ukanda huu inabadilika kwa kas ikiwemo uasi kaskazini mwa Msumbiji na hali ya kutokuwepo utulivu katika eneo la Maziwa Makuuna hivyo kufanya haja ya uwepo wa operesheni za ulinzi wa amani zilizo na ufanisi kuwa ya dharura zaidi kuliko wakati mwingine.
“Mafunzo haya yanakuja wakati ambapo ushirikiano kati ya wanajeshi, polisi na raia si tu wa muhimu bali ni wa lazima kwa ajili ya amani na usalama wa kudumu,” amongeza.
Brigedia Itang’are amesema kuwa programu hii inaakisi dhamira ya pamoja ya kuboresha maandalizi ya operesheni, kuendeleza usalama wa binadamu, na kuhakikisha kuwa operesheni za ulinzi wa amani ni shirikishi, za kimataifa na zinakabiliana ipasavyo na changamoto halisi.
Katika kipindi chote cha mafunzo haya, washiriki kutoka mashirika ya serikali, asasi za kiraia na vyombo vya ulinzi na usalama watashiriki katika masomo ya kina na mazoezi ya vitendo.
“Mitaala imeundwa ili kuimarisha si tu ujuzi wa kiufundi, bali pia maadili ya ushirikiano, kuheshimu tamaduni na kushirikiana na jamii—ambavyo vyote ni muhimu katika mazingira ya ulinzi wa amani,” alisema.
Amesisitiza kuwa mafunzo haya ni zaidi ya programu ya kawaida ya mafunzo, bali ni jukwaa la kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu na kuunda mtandao wa kikanda wa wajenzi wa amani ambao wataendeleza mafunzo hayo katika maeneo yao ya kazi.
Tanzania, ameongeza, kwa muda mrefu imekuwa ikitambulika kama kielelezo cha amani na utulivu katika ukanda huu, na imekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za amani za kikanda, ikiwemo ushiriki wa vijana katika operesheni za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Aidha, Tanzania inaendelea kuonesha dhamira thabiti ya kibinadamu kwa kuendelea kuwahifadhi wakimbizi wapatao 250,000 ndani ya mipaka yake.
Godfrey Mulisa, kutoka UNDP, alisisitiza pia kuwa Tanzania inasalia kuwa nguzo ya amani na utulivu katika ukanda huu kupitia uongozi wake, hasa katika maendeleo ya vijana na ushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani za kimataifa.
Alikiri kuwa mazingira ya usalama na amani ya kikanda yanaendelea kubadilika, huku tishio jipya na tata kama vile migogoro ya silaha kaskazini mwa bara likihitaji mbinu mpya na bunifu za kulinda amani.
“Mradi huu unalenga kuimarisha uimara wa kitaasisi wa kituo hiki, kupanua mafunzo kwa ajili ya nafasi muhimu za kiraia, na kuanzisha kozi za kisasa zenye mafunzo ya majaribio ili kuboresha utendaji katika shughuli za ulinzi wa amani,” alisema.
.jpeg)
Nomura Hiroyuki, akimwakilisha Balozi wa Japan nchini Tanzania, alisisitiza tena dhamira ya Japan katika mradi huu, akiuelezea kama ishara ya kweli ya urafiki na ushirikiano kati ya mataifa haya mawili.
“Japan na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa kirafiki kwa miaka mingi, hasa katika maeneo ya utamaduni na elimu,” amesema