Na Said Mwishehe,Michuzi TV
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kwamba chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, shirika hili limepanua wigo wake kupitia uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya ardhi na majengo, usimamizi mzuri wa miradi, pamoja na ushirikiano mpya kati ya sekta ya umma na binafsi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah Hamad, ameeleza hatua kwa hatua mafanikio ambayo yamepatikana kati ya mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2023/24.
Amesema kwamba mapato ya NHC yaliongezeka kutoka Shilingi bilioni 125 hadi Shilingi bilioni 189 ongezeko la asilimia 34 wakati huo huo amefafanua shirika lilipata jumla ya faida kabla ya kodi ya Sh.bilioni 235.4, ikiwa ni pamoja na Sh. bilioni 36.8 zilizopatikana katika mwaka wa fedha wa hivi karibuni, kwa mujibu wa ripoti zilizohakikiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ameongeza kuwa thamani ya mali za NHC pia iliongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia Sh trilioni 5.5 kufikia Juni 2024. Mchango wa shirika kwa hazina ya serikali nao umeongezeka, ambapo Shilingi bilioni 134.4 zimetolewa kama kodi kwa kipindi cha miaka mitano, pamoja na Sh.bilioni 9.85 kama gawio.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, NHC imetoa gawio la kihistoria la Sh bilioni 5.5, hatua iliyoliwezesha shirika hilo kupata pongezi kutoka kwa Rais kama moja ya mashirika ya umma yenye utendaji bora.”
Kwa upande wa ujenzi wa nyumba amesema
NHC imejenga nyumba 5,399 zenye thamani ya Shilingi bilioni 659.5 kwa ajili ya kuuza na kupangisha. Kati ya hizo, Hamad alisema, nyumba 3,217 zimekamilika, huku 2,182 zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mkurugenzi Hamad Abdallah Hamad ameitaja pia miradi maarufu ni pamoja na Morocco Square, ambayo hivi karibuni imekamilika baada ya kucheleweshwa kwa miaka mingi, na miradi ya Kawe 711 na Golden Premier Residence, ambayo sasa inaendelea tena kutokana na ufadhili kutoka kwa serikali.
“Shirika limefanikiwa kutekeleza mikataba ya kazi za umma 67 yenye thamani ya Sh.bilioni 458.2. Mikataba hiyo inajumuisha miradi ya kimkakati ya kitaifa kama vile Soko la Madini la Kimataifa la Tanzanite lililopo Mirerani, Kitengo cha Moyo cha JKCI jijini Dar es Salaam, na majengo ya wizara yaliyopo Dodoma.
“Kwa kushirikiana na washirika binafsi, NHC pia tumezindua miradi ya ubia 21 yenye thamani ya Sh.bilioni 351, ambayo imeongeza upatikanaji wa maeneo ya biashara na makazi kote nchini.
“Mafanikio ya NHC hayajapita bila kutambuliwa. Shirika limepokea tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa, zikiwemo za Mjenzi Bora wa Makazi ya Umma Afrika Mashariki, pamoja na pongezi kwa viwango vyake vya uandaaji wa taarifa za kifedha.
“Kupitia “Mpango wa Makazi wa Samia” unaolenga kutoa nyumba nafuu 5,000, pamoja na “Dhamana ya Nyumba” inayopendekezwa kwa ajili ya kukusanya mitaji kupitia uwekezaji wa umma, NHC iko tayari kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kukidhi mahitaji ya makazi yanayoongezeka nchini Tanzania.”
Ameongeza kuwa taswira ya kisasa ya mradi wa nyumba wa Kawe 711 unaoendelea kujengwa Kawe. Mradi huu utakuwa na huduma za biashara, makazi na michezo.
