Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 2.6 kati ya Shilingi bilioni 4.3 zilizoahidiwa na wadau mbalimbali kupitia kampeni ya Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya TET yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Aneth Komba alisema kampeni hiyo inalenga kuboresha hali ya upatikanaji wa vitabu vya kiada na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shule za sekondari nchini.
Dk Komba alisema kampeni hiyo inalenga kuboresha uwiano wa vitabu kwa wanafunzi kutoka kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu (1:3) kuwa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja (1:1) kwa kila somo na kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kutoa komputa mpakato kwa mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Wadau mbalimbali wa sekta binafsi, mashirika ya umma na watu binafsi waliguswa na kuchangia katika kampeni hii. Hadi kufikia juzi, TET imefanikiwa kukusanya fedha taslimu kiasi cha Sh 2,626,908,183 na ahadi zilizopokelewa toka kwa wadau mbalimbali juzi ni Sh 4,335,000,000,” alisema Dk Komba.
Aliwataja wadau waliochangia kuanzia Sh milioni 25 hadi Sh milioni 100 katika kampeni hiyo kuwa ni Nyambari Nyangwine Group of Companies (110,000,000), Mbesa Company Ltd (110,000,000), CI Group Ltd (100,000,000), Semuka International (100,000,000), Tanzania Printing Services (25,000,000) na Green Belt Investment (25,000,000).
Aliomba wadau kuendelea kuchangia kampeni hiyo katika kuhakikisha lengo la kitabu kimoja, mtoto mmoja inafikiwa na waweze kutimiza ndoto zao wakati wa ujifunzaji.
“Tunaamini kwa jitihada zetu za kutafuta rasilimali fedha tukichanganya na bajeti tunayopata toka kwa serikali yetu lengo la kitabu kimoja mtoto mmoja na komputa moja mwanafunzi mmoja kwa wanafunzi wa kidato cha tano litafikiwa,” alieleza.
Alisema wanathamini na kutambua mchango wa serikali katika uchapishaji wa kazi ya uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu hivyo wameona umuhimu wa kuunga mkono juhudi hizo kusaidia serikali kufika lengo la kila mtoto kupata kitabu kimoja.
Dk Komba alisema katika kipindi cha kati ya mwaka 2021 hadi 2024 TET iliandaa na kuchapisha vitabu nakala 5,872,825, kwa shule za wali, vitabu 15,076,976 kwa darasa la kwanza na la pili, vitabu 42,469,075 kwa darasa la III hadi VII, vitabu 6,860,244 kwa sekondari na vitabu 24,632 kwa vyuo vya ualimu.
Kadhalika, wamefanikiwa kuchapa na kusambaza nakala 600,000 vya maandishi makubwa na breli kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu ambavyo vimesambazwa kwa uwiano wa vitabu vitatu mwanafunzi mmoja.
” Vitabu hivi vimechapwa na kusambazwa kwa uwiano wa 1:3 kwa elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba pamoja na wanafunzi wa sekondari kwa masomo ya sanaa na lugha. Vitabu vya kiada vya masomo ya Sayansi (Hisabati, Fizikia, Kemia na Biolojia na masomo yote ya amali) huchapwa na kusambazwa kwa uwiano wa 1:1,” alieleza Dk Komba.