Dodoma, Juni 17, 2025 –
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi na mchango wake katika kukuza maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.
Waziri Simbachawene alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TAA katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, Dodoma, ambapo pia alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo kwa mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, Waziri Simbachawene ameelezwa kuhusu majukumu ya msingi ya Mamlaka ikiwa ni pamoja na kusimamia, kuendeleza na kuendesha viwanja vya ndege 61 vya serikali vikiwepo viwanja vya ndege viwili vya kimataifa vya Julius Nyerere na Kilimanjaro.
Aidha, Waziri Simbachawene alifahamishwa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa katika viwanja vya ndege vya Msalato, Tabora, Shinyanga, Musoma, Kigoma, Sumbawanga, Moshi na Lake Manyara
Akitoa maelezo hayo kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha ndege Msalato Jeff Shentiwa alielezea baadhi ya miradi yenye tija inayotekelezwa na TAA na kwa sasa imekamilika ikiwa ni pamoja na Mradi wa maboresho ya kiwanja cha ndege Iringa, Mtwara,Dodoma, Mpanda na Kahama.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Utoaji wa Huduma kwa Wananchi: Dhamira ya Mabadiliko ya Kiutawala Barani Afrika”, yakilenga kuhamasisha uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma zenye tija katika taasisi za umma.