
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo tarehe 20 Juni 2025.
SERIKALI imesema miradi 73 ya Biashara ya Kaboni imesajiliwa, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo tayari imeleta manufaa ya kiuchumi katika baadhi ya maeneo nchini huku shilingi bilioni 45 zimelipwa na kunufaisha wananchi katika halmashauri 10.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo tarehe 20 Juni, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Bernadeta Mushashu aliyetaka kufahamu biashara ya kununua na kuuza kaboni imeinufaishaje Tanzania.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis amesema miradi iliyosajiliwa ni ya sekta za misitu asilimia 51, nishati asilimia 33, taka asilimia tatu, kilimo asilimia nane na mifugo asilimia tano.
Akifafanua zaidi alisema utekelezaji wa miradi hii huchangia katika uhifadhi na urejeshaji wa misitu na ardhi, kuongeza fursa za ajira na pato la wananchi kwa ujumla na kupunguza uzalishaji wa gesi joto hivyo kufikia malengo ya utekelezaji wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Mhe. Khamis alisema fedha zilizolipwa katika halmashauri 10 nchini hutumika katika kutekeleza miradi ya kijamii katika vijiji husika kama vile ujenzi wa shule, zahanati, malipo ya bima za afya, ada za shule na chakula kwa wanafunzi.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge Bernadeta kuhusu vigezo vya kufanya biashara ya kaboni, Mhe. Khamis alisema mwekezaji anatakiwa awe na kampuni ambayo ameisajili na kupata eneo kwa ajili ya upandaji wa miti.
Aliongeza kuwa baada ya kupata eneo mwekezaji pamoja na ada ya usajili, anatakiwa aandae andiko na kuliwasilisha kwenye ofisi za Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro ili kupewa kibali cha utekelezaji wa mradi aliokusudia.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Khamis alibainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na maeneo mbalimbali itaendelea kutoa elimu na kuwaeleza fursa na faida za biashara ya kaboni wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Alisema hayo alipojibu swali la mbunge huyo aliyueliza lini Serikali itakwenda kuhamasisha wananchi wa Mkoa wa Kagera kuhusu biashara ya kaboni kwakuwa una misitu mikubwa kutokana na uwepo wa mvua za kutosha.
Aidha, Naibu waziri Khamis alisema Serikali inashirikiana kikamilifu na jumuiya ya kimataifa katika kubuni mikakati na hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote.
Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Nusrat Hanje aliyeuliza Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Asya Mwadini Mohammed.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Khamis alitaja baadhi ya mikakati iliyochukuliwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ikiwemo nishati safi ya kupikia ili kupunguza kasi ya ukataji wa misitu.
Mikakati mingine aliyoitaja ni kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris, kuandaa na kutekeleza nyenzo za kisera zinazotusaidia kutoa dira na kuibua programu na kutekeleza miradi inayosaidia jamii katika maeneo mbalimbali kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, alisema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini inayojumuisha upandaji miti, usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
Alitaja mikakati mingine kuwa ni ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi matuta na mabwawa kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira na urejeshaji wa maeneo ya ardhi yaliyoharibika.