Na Mwandishi Wetu, Sengerema
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema baada ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan Kuvunja Bunge Juni 27 mwaka huu,kazi iliyobakia kwa Chama hicho itakuwa ni kuendesha taratibu za kupata wagombea na kusisitiza haitaka mtu bali itateua.
Wasira ameyasema hayo leo Juni 24,2025 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wakati kihitimisha ziara yake katika mkoa huo..
Alifafanua wagombee wengi lakini watachuja na wala hawataka bali watateua kwani kuna tofauti ya kuteua na kukata.”Kukata ni kwa hasira,ukiteua unatazama uwezo kwa wakati.Kwahiyo CCM hatukati mtu ila tunateua wagombea wachache kati ya wanachama wengi.
“Maana tunawanachama wengi hivyo watakaobaki watasubiri uchaguzi mkuu mwingine maana vijana wako wengi.Hivyo wagombea wakiwemo Wabunge wanaomaliza muda wao watachukua fomu za kugombea na Julai 2 wanarudisha na baadae vikao vyetu vinawatazama vinapendekeza lakini tunataka kupendekeza wagombea wanaokubalika na wananchi.
‘Kwahiyo tunataka vikao vyetu vitege sikio wananchi wanasema nini kuhusu wagombea wanaotakiwa na baadae mnakuja kufanya uteuzi wa watu watatu na wapiga kura za maoni watapiga kura na wanatuletea mtu mmoja.Waliokuwa Bungeni hawatakuwa presha labda kama ulikuwa umewakimbia wananchi lakini uchaguzi umefika,”alisema Wasira.
Alisisitiza kwa wananchi wakiunge mkono Chama Cha Mapinduzi katika kuwapigia kura wagombea wao huku akisisitiza kuwa Chama chao hakikati wagombea bali kinateua na wananchi ndio wanachagua wagombea kwa kupiga kura.
Pia alisema tayari CCM wametimiza wajibu wao na wako tayari kwa uchaguzi mkuu na msimu wake ndio unaanza baada ya Rais kuvunja Bunge Juni 28 mwaka huu.
“Akivunja Bunge tunakuwa hatuna Bunge lakini tunakuwa na Rais kwasababu Serikali lazima iwepo, madiwani walishamaliza muda wao.CCM tulikutana Januari na tukasema kwa kazi nzuri iliyofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan tunampeleka akapeperushe bendera ya CCM kwa Watanzania…
“Ili tumpe mitano tena aendelee na kazi ya kuleta maendeleo ya nchi yetu kwani tumeona kazi aliyoifanya.Ndio maana tunasema mitano tena na Oktoba tuna TIKI,”alisema Wasira.