Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeingia kwenye
ushirikiano rasmi na Tanzania Startup Association (TSA) kwa kusaini makubaliano
ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuziwezesha biashara changa (startups)
kufikia masoko ya mitaji na kukuza mazingira ya ubunifu nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla iliyofanyika
katika ofisi za DSE jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi
kutoka taasisi zote mbili, wawakilishi wa vyombo vya habari pamoja na wadau wa
sekta ya mitaji na ubunifu.
Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa
Tanzania Startup Association, Ndg. Zahoro Muhaji, amesema ushirikiano huo ni
hatua muhimu kwa ekosistimu ya ubunifu nchini, hususan kwa vijana wenye mawazo
ya kibunifu lakini wanakosa maarifa au mitaji ya kuendeleza biashara zao.
“Makubaliano haya ni daraja la kuwaunganisha wabunifu wetu
na fursa rasmi za masoko ya mitaji. Ni mwanzo wa safari ya mabadiliko ya kweli
katika maendeleo ya biashara changa Tanzania,” alisema Muhaji.
Kwa upande wake, uongozi wa DSE umesisitiza kuwa ushirikiano
huo unalenga kuvunja dhana kwamba masoko ya mitaji ni kwa makampuni makubwa
pekee.
“Kupitia makubaliano haya, tunapanua wigo wa ushiriki wa
vijana, wabunifu na wafanyabiashara wadogo kwenye soko la mitaji. Tunajenga
mazingira jumuishi na endelevu ya uwekezaji,” ilieleza DSE.
“Makubaliano haya yanafungua ukurasa mpya kwa kizazi cha sasa na kijacho cha wafanyabiashara wa Kitanzania,” alisema Ndg. Zahoro Muhaji, Afisa Mtendaji Mkuu wa TSA, wakati wa hafla ya utiaji saini.
Kwa pamoja, DSE na TSA wamejipanga kuhakikisha mazingira wezeshi yanajengwa kwa ajili ya kuendeleza biashara zinazochipukia, kuongeza ujuzi wa kifedha na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.