Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti na wenye maono, ambao umeleta mageuzi ya kweli ya maendeleo kwa Taifa.
Akizungumza leo Alhamisi, tarehe 26 Juni 2025, wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la Kumi na Mbili, Dkt. Tulia amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Rais Samia amelihudumia Taifa kwa haki kwa kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ustawi wa jamii na kuimarika kwa huduma za msingi kwa wananchi.
Akitaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia, Dkt. Tulia alieleza kuwa Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma, Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo–Busisi) mkoani Mwanza, Mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Ujenzi wa hospitali za mikoa na rufaa, na Usambazaji wa huduma za elimu, maji safi na salama, pamoja na usambazaji wa nishati ya umeme vijijini na mijini.
“Tumeona umeme ukifika kule kwenye Vijiji, tumeona umeme ukifika kwenye mitaa. Na lipo hili lililomletea sifa Dkt. Samia na kuliletea sifa Taifa letu, Dkt. Samia ni kinara wa nishati safi duniani.” amesema Spika Dkt. Tulia Ackson.
Katika hotuba yake, Spika Tulia pia aliainisha miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika Jimbo lake la Mbeya Mjini, akiwemo Mradi wa Maji Kiwira, Barabara ya njia nne mjini Mbeya, Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo na usambazaji wa umeme katika kata 14 za pembezoni. Alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kulijali jimbo hilo na kumtakia kila la heri katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025.
Aidha, Dkt. Tulia alikumbusha kuwa tarehe 31 Mei 2025, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimtunuku Rais Samia Tuzo Maalum ya Heshima kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuwaletea maendeleo Watanzania. Tuzo hiyo imejumuika na msururu wa tuzo na Shahada za Udaktari wa Heshima alizozawadiwa na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kutokana na uongozi wake mahiri.