Tuzo ya Kiswahili ya SAFAL ya Fasihi ya Afrika imetangaza orodha fupi ya miswada iliyofuzu kwa mwaka 2024, ikionesha ushindani mkali kutoka kwa waandishi wa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Tuzo hiyo, inayodhaminiwa na kampuni ya Safal Group kupitia ALAF-Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya, imelenga kukuza na kuthamini fasihi ya lugha ya Kiswahili pamoja na lugha nyingine za Kiafrika tangu ilipoanzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree pamoja na Dkt. Mukoma wa Ngugi.
Akizungumza wakati wa kutangaza orodha hiyo, Mwenyekiti wa jopo la majaji, Dkt. Salma Hamad kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alisema kuwa licha ya idadi kubwa ya miswada iliyowasilishwa, kazi nyingi zilionyesha ubunifu wa hali ya juu.
“Miswada ilikuwa mingi, hata hivyo tumeburudika vya kutosha kwa sababu tumesoma kazi zilizoandikwa na kusukwa kiubunifu. Tumejifunza kwamba kuna hazina kubwa ya vipaji vya uandishi wa fasihi ya Kiswahili, ambavyo vikienedelezwa fasihi hii haitafilisika,” alisema Dkt. Salma.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Tuzo hiyo, Abdilatif Abdalla, alieleza kuwa ni jambo la kutia moyo kuona Tuzo ya SAFAL ikiendelea kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa waandishi wa mataifa mbalimbali kila mwaka, jambo linalochangia kukuza ubora na wigo wa fasihi ya Kiswahili.
Majaji wengine waliokuwa katika jopo hilo ni Prof. Richard Wafula kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya, na Dkt. Caesar Jjingo kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Jumla ya miswada 210 ilisomwa na kutathminiwa.
Miswada iliyotajwa katika orodha fupi ya mwaka 2024 ni kama ifuatavyo:
Riwaya
Nderemo za Mtaa – Joel Hamisi (Tanzania)
Kitanzi cha Mauti – Mayassa Abdallah Chembea (Tanzania)
Nyaraka za Wafu – Ali Othman Masoud (Tanzania)
Ushairi
Waadhi – Mohamed Hamid Haji (Tanzania)
Bure Ghali – Bashiru Abdallah (Tanzania)
Laana ya Uovu – Mohamed Idrisa (Tanzania)
Hadithi Fupi
Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine – Edwin Omindo (Kenya)
Kwa mujibu wa Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi, washindi wa mwaka huu watatangazwa katika hafla itakayofanyika Julai 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo inatoa zawadi ya jumla ya dola za Marekani 15,000 kwa miswada bora zaidi isiyochapishwa, katika tanzu za riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia na riwaya za michoro. Zawadi hizo zitagawanywa kama ifuatavyo:
Mshindi wa Kwanza (Riwaya) – Dola 5,000
Mshindi wa Kwanza (Ushairi) – Dola 5,000
Mshindi wa Pili (katika utanzu wowote) – Dola 2,500
Mbali na zawadi za fedha, miswada itakayoshinda katika mashindano haya pia itachapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, huku mashairi yatakayoshinda yakitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.
Safal Group imeendelea kuwa mdhamini mkuu wa Tuzo hii ya tisa mfululizo kwa kushirikiana na kampuni zake za Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo ya sanaa, utamaduni na lugha za Kiafrika.