Songea, Ruvuma
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amandius Jordan Tembo maarufu kama Toronto, leo tarehe 28 Juni 2026 amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Songea Mjini katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Toronto ambaye ni mwanachama hai mwenye rekodi ya utumishi uliotukuka kwa vitendo ndani ya chama hicho, amesema ameamua kuchukua fomu ili kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kutokana na kuona kuwa anaweza kuwa mwakilishi bora wa kusimamia na kuwatetea wananchi wa Songea.
Kwa mujibu wa Toronto, wakati umefika wa Jimbo la Songea kufanya mabadiliko ya kupata Mbunge ambaye yuko tayari kuwatumikia katika nyanja mbalimbali, huku msingi wa kwanza ukiwa ni kuboresha huduma za kijamii kwenye maeneo yote ya jimbo hilo.
Amesisitiza kuwa safari yake ya kisiasa bado haijafika mwisho na kwamba ni wakati wa yeye kulitumikia jimbo hilo kwa nguvu mpya kwa kuwa anaelewa changamoto zilizopo kwenye Jimbo la Songea Mjini kwa muda mrefu.
“Kwa heshima kubwa na unyenyekevu wa hali ya juu, nawajulisha kwamba rasmi leo tarehe 28 nimesimama mbele ya Wana Songea na Taifa kwa ujumla, kutangaza nia yangu ya kugombea Ubunge Jimbo la Songea kupitia Chama changu cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema Toronto.
Hii ni mara ya kwanza kwa Toronto kuwania Ubunge katika jimbo hilo na ni baada ya kutafakari kwa kina na kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu ujenzi wa jimbo hilo na Taifa kwa ujumla.
Katika kizazi cha sasa chenye ndoto nyingi lakini vitendo vichache, jina la Amandius Jordan Tembo maarufu kama Toronto linaibuka kama ishara ya matumaini mapya katika siasa za Tanzania.
Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 35 na elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada, Toronto ameamua kurejea nyumbani Songea, Ruvuma, kwa lengo la kuchangia maendeleo ya jamii na kukuza thamani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama anachokipenda kwa dhati.
Toronto amejiwekea malengo ya kuhakikisha kila kata ndani ya Manispaa ya Songea inakuwa na ofisi ya kisasa ya CCM. Tayari amefanikisha ujenzi wa ofisi mbili Tawi la Liwena Kata ya Subira na Kata ya Bombambili kwa kutumia fedha zake binafsi.
Ujenzi wa ofisi ya Bombambili uliogharimu zaidi ya Sh milioni 30, ulifanyika kwa miezi mitatu na kukabidhiwa rasmi kwa uongozi wa chama, jambo lililopokelewa kwa pongezi kutoka kwa viongozi na wananchi.
Kwa Toronto, kujenga miundombinu ya chama ni sawa na kujenga jamii. Anasisitiza kuwa maendeleo hayawezi kusubiri serikali pekee, bali kila mwananchi ana jukumu la kuchangia. Kwa maono yake, Songea inapaswa kuwa mfano wa mafanikio yatokanayo na mshikamano wa jamii na jitihada binafsi za wazalendo.
Mbali na siasa, Toronto pia anashiriki katika miradi ya kijamii kama elimu na uwezeshaji wa watoto, akiamini kuwa moyo wa kujitolea na kugusa maisha ya watu huongeza mshikamano, kwamba mabadiliko huanza na dhamira ya kweli na uzalendo.
Toronto anaendelea kuhamasisha vijana kushiriki katika siasa ya vitendo na siyo kauli. Jitihada zake zimeleta hamasa mpya kwa vijana ndani ya CCM na kumfanya kuwa mfano wa kizazi kipya cha viongozi wenye maono, vitendo na uzalendo.