NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Tumaini Nagu amewakumbusha Wadau, Makatibu Tawala Mikoa,Maafisa lishe na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa kwenda kuendelea kutekeleza Program ya Kitaifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kikamilifu ili kuwezesha watoto kukua na kufikia utimilifu wao,kutimiza ndoto pamoja kuwa na mchango katika Taifa.
Prof. Nagu ameyasema hayo leo hii Jijini Dodoma Julai 2,2025 wakati akifungua Kikao kazi cha Uwasilishaji wa Viashiria vya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECDI 2030)
Pamoja na kuwataka kuhakikisha Program hii inatekelezwa katika ngazi zote ikiwemo Mikoa,Halmashauri na ngazi ya Jamii.
Bila kusahau kutenga bajeti ili kuchochea utekelezaji wa Program hii ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwenye ngazi zote kuanzia Mikoa na Halmashauri.
“Ndugu Washiriki nitumie fursa hii kuwakumbusha kwenda kuendelea kutekeleza program hii ya Kitaifa kwa ukamilifu ili kuwawezesha watoto wetu kukua na kufikia utimilivu wao na ndoto zao zitimilike na pia wawe na mchango katika Taifa letu”.
Awali akitoa salamu za Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Mwakilishi wa Shirika hilo Bwana Abbas Mtemba amesema kuwa kama Taifa kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha watoto wanakuwa katika hali ya kufikia utimilifu unaokusudiwa hasa katika masuala ya Afya,Kujifunza,Saikolojia na ya Jamii.
Pamoja na kuahidi kuwa Unicef itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha mifumo ya Kiserikali inawezesha watoto na jamii kupata huduma bora na stahiki za Malezi.
“Kama ambavyo tutaona katika Matokeo,Sisi kama Taifa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa katika ile hali ya kufikia utimilifu unaokusudiwa hasa katika masuala ya Afya,Kujifunza,Saikolojia na Jamii,ambapo hili likifanyika vizuri itachangia baadae kuwa na kizazi au jamii yenye tija kubwa”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) Bi Mwajuma Kibwana amesema kuwa Tafiti zinasema ni asilimia 47 tu ya watoto wa miezi 24 hadi 59 walioko katika hatua za ukuaji timilifu ambao ni chini ya miaka 5 huku asilimia 53 wakiwa bado wanalega lega kwenye eneo hili la makuzi,Malezi na Maendeleo ya awali ya mtoto.
Sambamba na kuiomba Serikali pamoja na wadau wake mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanaboresha hali za watoto ili kuwa na Taifa lenye Tija.
Kikao kazi hiki kimehuduriwa na Wadau mbalimbali wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto,Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Mikoa 15,Maafisa lishe na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa.