Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Wafanyabiashara na Wawekezaji mbalimbali wa Uhispania katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Wafanyabiashara wa Uhispania lililofanyika Jijini Sevilla nchini Uhispania leo tarehe 02 Julai 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Wafanyabiashara na Wawekezaji mbalimbali wa Uhispania mara baada ya Jukwaa la Biashara la Tanzania na Wafanyabiashara wa Uhispania lililofanyika Jijini Sevilla nchini Uhispania leo tarehe 02 Julai 2025.
Wafanyabiashara, Wawekezaji mbalimbali wa Uhispania pamoja na Viongozi wa Sekta ya Uwekezaji nchini Tanzania wakishiriki Jukwaa la Tanzania na Wafanyabiashara wa Uhispania lililofanyika Jijini Sevilla nchini Uhispania na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 02 Julai 2025.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Tanzania ipo tayari kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya wafanyabiashara wa Uhispania kwa kuwa Tanzania na Uhispania zinaweza kuunda ushirikiano wa kiuchumi wenye nguvu ili kuimarisha diplomasia ya kiuchumi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Jukwaa la Biashara la Tanzania na Wafanyabiashara wa Uhispania lililofanyika Jijini Sevilla nchini Uhispania leo tarehe 02 Julai 2025. Amesema Tanzania bado inaitambua Uhispania kama mshirika muhimu katika sekta za kimkakati kama vile nishati mbadala, miundombinu, teknolojia ya kilimo, utalii, viwanda vya rasilimali za baharini na biashara.
Makamu wa Rais amesema Tanzania inatambua sekta ya binafsi kama mshirika mkuu katika juhudi za maendeleo inayoongoza katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali zilizopo.
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba Tanzania ni Taifa lenye utulivu wa kisiasa, eneo la kimkakati la kijiografia, maliasili nyingi, idadi kubwa ya vijana pamoja na uchumi unaokua kwa kasi. Ameeleza utekelezaji wa mageuzi unaofanywa na serikali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutambua nafasi muhimu ya sekta binafsi katika maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais amesema chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Serikali imeimarisha mifumo ya sheria, miundombinu ya kisasa na kuweka dhamira thabiti ya uwazi na utawala bora. Ameongeza kwamba kwa sasa Tanzania ni kivutio cha uwekezaji katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika huku ikitoa fursa katika sekta muhimu kama vile biashara ya kilimo, utalii, nishati, madini, viwanda, uchumi wa bluu, na miundombinu.
Makamu wa Rais amewakaribisha kuwekeza katika maeneo ya kimkakati ikiwemo teknolojia ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya mkaa na kuni. Amesema eneo lingine la uwekezaji ni uvunaji wa rasilimali za uchumi wa bluu katika Bahari ya Hindi pamoja na Maziwa Makuu.
Ametaja maeneo mengine ni pamoja na uvuvi na usindikaji, uchunguzi wa madini, utalii wa pwani na baharini, usafirishaji pamoja na uwekezaji katika kuendeleza maeneo ya pwani ya Tanzania na visiwa ili kunufaika na rasilimali za uchumi wa bluu na uhifadhi wa mazingira.
Katika Mkutano huo Viongozi wa Sekta ya Uwekezaji wamewasilisha maeneo mbalimbali ya kuwekeza nchini Tanzania pamoja na kuonesha mageuzi mbalimbali yaliyofanyika nchini ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Pia wameeleza fursa za uwepo wa soko la uhakika wa bidhaa kutokana idadi ya watu, eneo la kijiographia la Tanzania ambalo linahudumia nchi mbalimbali, uboreshaji wa miundombinu ya msingi pamoja na maendeleo makubwa katika sekta ya TEHAMA.
Jumla ya Makampuni 31 yameshiriki katika Mkutano huo ambayo yamejikita katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo chakula na kilimo, ujenzi wa miundombinu, viwanda, sekta maji, sekta ya madini, nishati, TEHAMA, utalii pamoja na sekta ya fedha.
Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Aboud Mwinyi, Balozi wa Tanzania nchini Hispania mwenye Makazi yake nchini Ufaransa Mhe. Ali Mwadini, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Gilead Teri, Meneja wa Uwekezaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Omary Omary, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi Raphael Maganga, Katibu wa Baraza la Biashara Tanzania Dr. Godwill Wanga pamoja na Kamishna wa Fedha za Nje Wizara ya Fedha Rished Bade.
.jpg)