Farida Mangube, Morogoro.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata watu saba wanaodaiwa kuhusika na tukio la utekaji na mauaji ya Bernad Masaka (43), mfanyabiashara maarufu wa maduka ya nyama na Katibu wa Wachinjaji wa Nyama Mkoa wa Morogoro, aliyepotea Juni 1, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 3, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi Alex Mkama, amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa Masaka alitekwa na Stanley Ng’ambi maarufu kwa jina la Jaja (31), ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mkundi, akiwa anaendesha gari aina ya Toyota Premio.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, Ng’ambi akiwa na wenzake walimrubuni Masaka kuwa wanakwenda eneo la Makunganya kwa ajili ya kununua ng’ombe wa biashara. Hata hivyo, mara baada ya Masaka kuingia ndani ya gari, walimuua kwa kutumia silaha kali kisha kuuchukua mwili wake na kuutupa katika eneo la Majengo, Kijiji cha Manga, Kata ya Mkata, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Kamanda Mkama amesema uchunguzi unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kibiashara. Baada ya kukamatwa, watuhumiwa walikiri kuhusika na kuwaongoza askari hadi eneo walipotupa mwili wa marehemu. Vilevile, polisi wamefanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Premio lililotumika katika uhalifu huo pamoja na pikipiki aina ya Boxer iliyokuwa inamilikiwa na marehemu.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Stanley Ng’ambi maarufu Jaja (31), Bahati John (44), Japhet Michael (29), Yusuph Mkamba (27), Nickson Ibrahim (43), Robson Rite (47) na Ernest Msiet (37).
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa kina unaendelea huku taratibu za kisheria zikiendelea ili kuhakikisha haki inatendeka kwa familia ya marehemu na wahusika kufikishwa mahakamani.