📌 Asisitiza milango ya Rais Samia ipo wazi kwa ajili ya mazungumzo kwa mustakabali wa Taifa
📌 Asema Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Taasisi za dini
📌 Serikali kuendelea kushirikiana na Taasisi za dini kuchochea maendeleo
📌 Uchaguzi ni daraja la amani na maendeleo si chanzo cha mifarakano – Baba Askofu Shoo
📌 CCT yahimiza maadili ya kisiasa, utulivu wa jamii na kampeni za kistaarabu
📌 Taasisi za dini Afrika zatajwa kuchangia maendeleo ya sekta ya afya kwa 30%- 70%
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini kwa kuwa anawaongoza wananchi wenye dini ambao dini zao wanaziheshimu na hivyo asingependa kuona haki zao zinanyimwa kwa namna yoyote ile.
Dkt. Biteko amesema hayo Julai 3, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
“Mheshimiwa Rais Samia anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini na ninyi ni mashahidi amekuwa akiwaalika ili tuzungumze masuala mbalimbali ya kitaifa ingekuwa ni mtu anayejifungia ndani na akasema analo jeshi, sheria, katiba na vyombo vya ulinzi basi nitafanya kazi nadhani hivi ingekuwa ngumu sana lakini yeye amesema milango yetu iwe wazi tuzungumze na viongozi wa dini kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa nchi yetu pale ambapo tunadhani hatuendi sawasawa,” amesema Dkt. Biteko.
Akijibu hoja za CCT, Dkt. Biteko amesema kuwa imekuwa desturi ya nchi kuwa na waangalizi wa ndani kwenye Uchaguzi Mkuu na kuwa ni imani yake kuwa Tume Huru ya Uchaguzi itawalika waangalizi wa ndani ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia. Hata hivyo amesisitiza Tume Huru ya Uchaguzi iachiwe uhuru wake wa kufanya kazi zake.
Amewahakikishia kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na taasisi zote za dini ikiwemo makanisa na kusema kuwa tangu Uhuru mwaka 1961, Taasisi za dini zimeendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwanufaisha watu wengi kote nchini.
“Tunawapongeza sana na tunawashukuru sana kwa mchango wenu. Tafiti zinaonesha kuwa Taasisi za dini Barani Afrika huchangia kati ya asilimia30 hadi 70 ya maendeleo ya sekta ya afya. Kidunia, kwa mfano katika elimu, Vyuo kama University of Edinburgh – (Scotland), Oxford University – Uingereza na University of Kwa Zulu – Natal Afrika ya Kusini vilianzishwa na Taasisi za dini,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kuzungumzia mchango wa taasisi za dini katika kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali duniani ambao wanaendelea kuiokoa dunia kutoka katika matatizo na majanga mbalimbali akitolea mfano Tasisi ya World Coucil of Churches na World Vision kwa kutoa huduma za kibinadamu duniani kote bila kubagua tofauti zilizopo za dini, rangi, kabila na jinsia.
Katika kutambua mchango wa viongozi wa dini Afrika na duniani kote, Dkt. Biteko ameelezea haiba ya Mwanatheolojia Muanglikana kutoka Afrika Kusini, Hayati Baba Askofu Desmund MpiloTutu kama kiongozi wa dini mwenye upendo, mpendahaki na amani, ambaye amechangia kutetea haki za binadamu na kupambana dhidi ya u baguzi na hivyo kusaidia kuleta maendeleo na usawa kwa nchi ya Afrika Kusini na dunia kote.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikistro Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Fredrick Shoo amepongeza usikivu wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za Serikali za kudumisha demokrasia kwa kuruhusu mikutano ya hadhara sambamba utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Baba Askofu Dkt. Shoo amesema CCT inahimiza maadili ya kisiasa na utulivu wa jamii ikiwa ni pamoja na kampeni zisizo za kuvunjiana heshima bali zinazoweka mbele maslahi ya Taifa na kupinga vitendo vyote vya rushwa.
“ Uchaguzi ni daraja la amani na maendeleo si chanzo cha mifarakano, jamii idumishe amani, mshikamano na uzalendo wa kila mmoja kwa nafasi yake. Pia Tume Huru ya Uchaguzi iendelee kusimamia haki kwa kushirikiana na waangalizi wa ndani amesema ,” Baba Askofu Shoo.
Amebainisha kuwa CCT itaendelea kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya jamii hivyo ameiomba Serikali itoe unafuu wa kodi na kutotoza ruzuku kwa misaada inayotolewa na wahisahi ili kuboresha ubora wa huduma na kuwafikia wananchi.
Katibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dkt. Moses Matonya amesema kuwa CCT ni Jumuiya inayounganisha madhehebu wanachama 12 na mashirika ya kikristo 14. Aidha katika Mkutano huo jumla ya wajumbe waliohudhuria ni 224 kati ya wajumbe wote 280.