Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MKURUGENZI wa Masoko kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Frank Nyarusi, amesema kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza pato la taifa, na kutoa wito kwa Watanzania—hasa vijana—kuchangamkia fursa lukuki zilizopo katika sekta hiyo.
Akizungumza kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Nyarusi amesema kuwa licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa kahawa barani Afrika, kiwango cha matumizi ya kahawa nchini bado ni kidogo, jambo linalochangiwa na upotoshaji wa taarifa kuhusu faida za kahawa kiafya na kijamii.
“Kuna makampuni mengi yanayotengeneza kahawa, lakini sisi tupo hapa kuwaelimisha Watanzania kuhusu utengenezaji wa kahawa bora na faida zake. Watu wengi bado hawanywi kahawa kwa sababu wamepewa taarifa zisizo sahihi,” amesema Nyarusi.
Ameeleza kuwa jukumu kuu la TCB katika maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa zao la kahawa kwa afya, uchumi na biashara, na kuwaonesha Watanzania—hasa vijana—namna wanavyoweza kushiriki kwenye mnyororo wa thamani wa zao hilo bila hata kulima.
“Si lazima mtu aende shambani ili kupata kipato kupitia kahawa. Kupitia mradi wa ‘Kahawa Mkono’, tumewapa vijana bajaji maalum zilizo na vifaa vya kuuza kahawa mitaani. Tumewasaidia pia kuunganishwa na benki ili kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuanzisha biashara,” alifafanua.
Amesema mkakati huo unalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya kahawa, ikizingatiwa kuwa zao hilo lina masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi, na linamlinda mkulima kupitia mfumo wa bei elekezi.
“Kahawa inalipa. Ndiyo maana tumepanda kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu Afrika kwa uzalishaji wa kahawa, tukizipita nchi kama Kenya. Lengo letu ni kuwa wauzaji wakuu wa kahawa Afrika,” amesema kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa Tanzania ina ardhi na mazingira yanayofaa kwa uzalishaji wa kahawa aina mbalimbali, hali inayowezesha nchi kuzalisha kahawa bora kwa ajili ya soko la kimataifa.
“Tupo tayari kuhudumia dunia nzima kwa kikombe bora cha kahawa ya Tanzania,” amesema.
Kuhusu uzalishaji wa miche ya kahawa, Nyarusi amesema TCB kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa miche kutoka 6,000 hadi zaidi ya 31,000, huku lengo likiwa ni kufikia miche milioni 40 itakayogawiwa bure kwa wakulima kote nchini.
“Tunawaomba wakulima wachangamkie fursa hii kwa kuongeza mashamba yao, kwani kahawa ni furaha ya mkulima,” amesema.
Amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa na kuhakikisha ubora wa mazao yao ili kuhimili ushindani wa soko la kimataifa na kunufaika zaidi kiuchumi.