Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar.
KATIKA juhudi za kusukuma mbele mageuzi ya sheria za habari zinazotajwa kuwa kandamizi na zilizopitwa na wakati, wadau kutoka Kamati ya Kuratibu Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) leo wamekutana na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika ukumbi wa TAMWA-Z uliopo Tunguu.
Mkutano huu umekuwa jukwaa la wazi la kutoa hoja, kueleza changamoto, na kuomba ushirikiano wa kweli kutoka kwa wawakilishi katika kuhakikisha Zanzibar inapata sheria bora, rafiki na za kisasa kwa waandishi wa habari.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Z, Dk. Mzuri Issa, amesema kuwa ni wakati wa Zanzibar kutengeneza mazingira bora kwa waandishi wa habari “Tunataka Mazingira Salama kwa Waandish,”.
Mjumbe wa Kamati ya Kitaalamu ya Masuala ya Habari kutoka ZAMECO, Shifaa Said, amesema kuwa hoja ya mabadiliko ya sheria si ya kundi moja tu, bali ni suala la kitaifa linalohitaji ushiriki wa kila mmoja.
“Sheria hizi zimekaa kwa muda mrefu bila kufanyiwa marekebisho. Tunahitaji nguvu za pamoja ili kuhakikisha tunawalinda waandishi wetu, hasa wakati wa uchaguzi,” amesema Shifaa Said
Sambamba na hayo amesisitiza kuwa ushirikiano wao na wawakilishi ni mkubwa, lakini sasa wanaona ni lazima suala hilo libebwe na jamii nzima. “ Sheria hizi zinawahusu wananchi wote kupitia habari,” alisisitiza.
Kwa upande wake Abdallah Mfaume, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar na mjumbe wa ZAMECO, amesema kuwa sheria za sasa hazilindi waandishi wala kutambua changamoto za habari katika karne ya 21.
“Waandishi hawana uhakika wa usalama wao, hususan katika vipindi nyeti vya uchaguzi. Tunahitaji sheria mpya zenye kulinda haki na uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.
Prof. Omar Fakih, Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, ameeleza kuwa serikali haijawahi kupinga haja ya mabadiliko ya sheria hizo, lakini changamoto zimekuwepo kwenye hatua za kuwasilisha muswada husika.
“Niliomba muswada huu uwasilishwe rasmi. Kuna ucheleweshaji, lakini kuna nia. Tunapaswa kuendeleza msukumo huu,” ameeleza.
Aidha Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman, amekiri kuwa hoja ya mabadiliko ilijadiliwa kwa kina ndani ya Baraza, lakini kuchelewa kwa muswada huo kusomwa rasmi kumeleta masikitiko.
“Ni muhimu tusigawanyike kwenye makundi. Umoja wetu ndio silaha yetu. Serikali itafanya marekebisho, lakini tuvute subira,”
Pamoja na hayo Mwanasheria kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Shadida Omar, amesisitiza umuhimu wa mashirikiano ya kisheria na kiusalama kwa waandishi.
“Tunaendelea kuhimiza ulinzi wa waandishi kipindi cha uchaguzi, huku tukifuatilia mchakato wa muswada wa sheria kwa karibu,” amesema.
Nae Hawra Shamte, Mwenyekiti wa Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar, ameeleza kuwa juhudi za kutoa mafunzo kwa waandishi juu ya haki na sheria zimekuwa endelevu ,“Tunatoa mafunzo kuhusu sheria za habari, usalama wa waandishi na namna ya kuripoti uchaguzi. Lakini yote haya hayana nguvu bila sheria bora,” amesema.
Hata hivyo, mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Dr. Mohamed Suleiman amehitimisha kwa kusema kuwa wawakilishi wako tayari kuendelea kuwasilisha hoja ya sheria kwa manufaa ya taifa.“Tutazidi kuishauri Serikali kwa nia njema, suala hili si la waandishi tu, bali ni la haki ya wananchi kupata habari sahihi,” ameeleza.