Na: Calvin Edward Gwabara – Dar es salaam.
Kamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala bora Bwana Nyanda Shuli amepongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu
wa Sheria OCPD kwa kufanyia kazi mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbalimbali
za nchi ambayo yanaibuliwa na Wananchi kwenye maeneo mbalimbali.
![]() |
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Bwana Nyanda Shuli akipata maelezo kutoka kwa Bi Happyphania Luena kutoka OCPD. |
Pongezi hizo amezitoa wakati
alipotembelea banda la Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwenye maonesho
ya Kimataifa ya Biashara SABASABA yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwl Julius
Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam.
“Ofisi hii inatoa huduma ambazo
zinaelekeana sana na zetu, maana sisi tunapokea mapendekezo mbalimbali kutoka
kwa wadau na wananchi kuhusu sheria zetu nchini na baadae zinapitia michakato
mbalimbali lakini mwisho wa siku lazima zipite kwenu kwaajili ya kuandika na
kuzifanyia mabadiliko kabla ya kupelekwa bungeni ili zipitishwe, na kwa maana
hiyo tunashirikiana katika kuwezesha haki na sheria zinakwenda na wakati”
alifafanua Kamishna Shuli.
Aliongeza “Kuna kipindi tulienda
Mikoa ya kusini kwenye uchunguzi fulani, tukakutana na Jaji Mfawidhi wa Kanda
ya Kusini akatuambia jamani tusaidieni kwani kuna sheria tunazitumia hapa
lakini ukizitazama tunaona kwa mazingira ya utungwaji wake na mazingira yetu
zimeenda zaidi wakiitaja sheria ya Uhujumu uchumi inagusa kwato za swala na
pembe za digidigi kuwa ni uhujumu uchumi lakini tunaona kipindi kile sheria
ililenga kulinda wale wanyama “ Big 5” wasipotee lakini sheria ikaingiza swala
na digidigi na sasa tuna watu wengi Magereza kwa kesi hizo na hawapewi dhamana”
.
Kamishna Shuli amesema anashukuru
baada ya mchakato mrefu wa maoni hayo sheria hiyo ilifanyiwa mabadiliko na
kuiweka kulingana na matakwa halisi ya malengo ya serikali kwa maslahi mapana
ya taifa tofauti na ilivyokuwa awali na hapo ndipo unapoonekana umuhimu mkubwa
wa Ofisi hii lakini pia ushirikiano uliopo katika utekelezaji majukumu.
Kwa upande wake Mwandishi wa Sheria
toka OCPD Bi. Happyphania Luena amemshukuru Kamishna kwa kutembelea banda hilo
kujifunza kazi za Ofisi hiyo lakini ametambua mchango na ushirikiano walio nao
kati ya OCPD na Tume hiyo ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika
kuhakikisha haki na masula ya kisheria yanazingatiwa katika jamii.
“Mbele yako ni Juzuu za Sheria
zilizofanyiwa Urekebu toleo la mwaka 2023 tumezileta hapa kuwaonesha wananchi
na kuwalewesha kwanini toleo la mwaka 2002 limefutwa baada ya kuzindualiwa hili
la mwaka 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia SUluhu
Hassan lakini pia tunawapa elimu wananchi umuhimu wa kazi hii ya urekebu wa
sheria zetu” alieleza Bi Happyphania.
![]() |
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Bwana Nyanda Shuli akioneshwa Juzuu za Toleo la Urekebu wa sheria la mwaka 2023. |
![]() |
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Bwana Nyanda Shuli akiangalia na kufurahia kitabu cha majina ya Sheria zote za nchi zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. |
![]() |
Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA bwana John Pumbalu alipotembelea banda la OCPD. |
![]() |
Wanafunzi wakipata maelezo kuhusu mchakato wa utungwaji wa sheria kwenye banda la OCPD. |