Katika zama hizi ambapo Afrika inapambana kufungua milango ya maendeleo kupitia biashara, nishati na uwekezaji, mkutano wa Afrika Unlocked 2025 uliofanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini, umeibua dira mpya ya namna bara letu linaweza kujiinua kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake lenyewe.
Mkutano huo wa siku mbili, ulioratibiwa na Benki ya Standard Bank ambayo ni benki mama ya Stanbic Bank Tanzania, uliwakutanisha viongozi kutoka sekta binafsi, serikali, mashirika ya kifedha na wajasiriamali kutoka zaidi ya mataifa 20.
Lengo kuu lilikuwa kujadili kwa undani jinsi Afrika inaweza kujenga uchumi wa pamoja unaojitegemea na wenye ushindani kimataifa.
Katika mijadala mbalimbali, mada tano kuu zilipewa uzito wa kipekee: kuimarisha biashara ya ndani kupitia Mkataba wa Biashara Huria Barani Afrika (AfCFTA), kuboresha miundombinu ya bandari, barabara na reli, kupanua upatikanaji wa nishati safi na salama, kuongeza mitaji kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), na kuwekeza zaidi katika kilimo na uongezaji thamani mazao.
Kwa Tanzania, hizi si mada mpya, ni changamoto na fursa halisi zinazoonekana kila siku. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye nafasi ya kuwa kitovu cha biashara ya kikanda kutokana na jiografia yake na uwekezaji unaoendelea katika bandari ya Dar es Salaam, reli ya kisasa ya SGR na barabara kuu zinazounganisha nchi jirani.Katika sekta ya kilimo, maeneo ya nyanda za Juu Kusini yameonyesha uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya mafuta kama alizeti na soya.
Hata hivyo, ukosefu wa mitaji na teknolojia ya uchakataji bado unazuia wakulima kunufaika ipasavyo.“Mkutano huu umetufumbua macho. Tunahitaji kujenga mifumo ya kuaminiana, kupunguza utegemezi wa masoko ya mbali, na kutumia soko la Afrika lenye zaidi ya watu bilioni moja,” alisema mwakilishi mmoja wa sekta ya viwanda kutoka Afrika Mashariki.
Washiriki wa mkutano pia waligusia umuhimu wa taasisi za kifedha, kama benki za biashara, kubadilisha mikakati yao ili kuwa karibu zaidi na biashara za familia na SMEs kwa kuzingatia kuwa ndizo zinachochea ajira na ukuaji wa uchumi.
Pamoja na changamoto zilizopo kama gharama za usafirishaji, vikwazo vya forodha na ukosefu wa miundombinu bora katika baadhi ya maeneo, ujumbe kutoka Afrika Unlocked ni wazi: Afrika inaweza kuwekeza ndani yake, kujenga masoko ya ndani na kukuza uwezo wa uzalishaji bila kutegemea nje.
Kwa Tanzania, huu ni wakati wa kutafsiri dira hiyo ya bara kwa vitendo — kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuimarisha mazingira ya biashara, na kutumia fursa ya AfCFTA kufungua milango ya masoko mapya kwa wazalishaji wa ndani.