-Wasira akabidhi kwa niaba ya Rais Samia
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa sh. milioni 50 kuchaia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Nyalikungu wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu.
Akiwasilisha mchango kwa niaba ya Rais Samia, wilayani Maswa, jana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alisema Dk. Samia anatambua mchango wa viongozi wa dini katika kuimarisha umoja na amani ya nchi.
“Sasa nawapa salamu za Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Rais Dk. Samia na kwa sababu nilimwambia nimealikwa mahali hapa kuwa mgeni rasmi kwa ajili ya mchango wa Kanisa na yeye ni mchamungu akaniambia na yeye atachangia sh. milioni 50,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, aliwaomba viongozi wa kanisa kuendelea kuiombea nchi hususan katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu ufanyika kwa uhuru na amani.
“Naamini kabisa kwamba mnafahamu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, tunaliomba kanisa, tunawaomba viongozi wetu wa kanisa, tunawaomba waumini wote tuliombee taifa letu tunapopita katika uchaguzi huu kukawe na uchaguzi wa amani uchaguzi ulio huru lakini zaidi uchaguzi utakaotupatia viongozi watakaoendelea kuliongoza taifa hili,” aliomba.
Akitoa salamu za shukrani Paroko wa Parokia hiyo, Padri Deogratius Ntindiko, alimshukuru Rais Samia kwa kuguswa na ujenzi huo na kuchangia kiasi hicho cha fedha.
“Kupitia nafasi yako (Wasira) tunamshukuru sana Rais Dk. Samia amegusa nyoyo zetu amegusa matarajio yetu kwa mchango wake wa sh. milioni 50, sisi wana Nyalukungu tunamuombea,” alisema.