Kassim Nyaki, NCAA.
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) inatumia fursa ya mkutano wa pili wa mabaraza huru ya Habari Afrika unaofanyika jijini Arusha kunadi vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro ili kuendelea kuwavutia wageni wengi zaidi.
Mkutano huo unaofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 14- 17 Julai 2025 unawakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Habari kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika ambapo washiriki zaidi ya 200 wanahudhuria mkutano huo.
Afisa Utalii Mkuu NCAA Peter Makutian ameeleza kuwa ushiriki wa NCAA katika mkutano huo unalenga kuwafikia wajumbe wa mkutano huo na kuwaelezea vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro ambayo ni kivutio Bora cha Utalii Afrika kwa mwaka 2023 na mwaka 2025.
“Kama mnavyojua Ngorongoro ni kivutio Bora cha utalii Afrika hivyo wageni wanahamasika na kuwa na shauku ya kujua vivutio vilivyopo, fursa za uwekezaji na shughuli za utalii, kwa siku zote za mkutano huu tutahakikisha tunawafikia na kuendelea kutangaza eneo letu” alisema Makutian.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni; “Kuendeleza kanuni za vyombo vya habari na mawasiliano kwa ubora wa uandishi wa habari barani Afrika”