WACHEZAJI watano wa gofu wameibuka washindi katika mashindano ya Lina PG Tour yaliyofanyika katika viwanja vya Lugalo Golf Club, jijini Dar es Salaam, kuanzia Julai 17 hadi 20, 2025.
Mashindano hayo ambayo yalihitimishwa majira ya jioni, yalikutanisha wachezaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiwemo wa kulipwa, wa ridhaa na chipukizi.
Kwa upande wa wachezaji wa kulipwa, Fadhili Nkya kutoka Klabu ya Gymkhana Dar es Salaam ameibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia zawadi ya Shilingi Milioni 6.8. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Abdallah Yusuph aliyepata Shilingi Milioni 4.3, huku mshindi wa tatu akiwa ni Nuru Mollel aliyejishindia Shilingi Milioni 3.4.
Katika kundi la wachezaji chipukizi (Elites), Prosper Emmanuel ameibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza na kupata Shilingi Milioni 2.2. Nafasi ya pili imegawanywa na Julius Mwinzani pamoja na Gabriel Abel baada ya kufungana kwa pointi, na kila mmoja kujinyakulia Shilingi Milioni 1.1.
Kiongozi wa wanawake wacheza gofu jijini Dar es Salaam, Bi. Chiku Elias, ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano ya gofu ili kukuza idadi ya wachezaji wa mchezo huo nchini. Aidha, amewashukuru wote walioshiriki katika mashindano ya Lina PG Tour kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa.
“Hii inatia hamasa sana kuona mashindano haya yanavutia wachezaji na mashabiki wengi. Hata hivyo, bado tunahitaji kuona idadi hiyo ikiongezeka zaidi,” alisema Bi. Chiku.
Aliongeza kuwa mashindano haya yamehusisha wachezaji kutoka mikoa mbalimbali kama Dar es Salaam, Moshi, Morogoro na Arusha, ikiwa ni sehemu ya awamu ya tatu ya mashindano hayo.
“Kwa kweli maandalizi ya mashindano haya yamekuwa bora, hatujawahi kuona makosa makubwa kutoka kwa waandaaji. Tuna matumaini kuwa mashindano yajayo yatakuwa makubwa zaidi, kulingana na yatakapofanyika,” aliongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashindano na Mkuu wa familia ya Nkya, Bw. Said Nkya, alisema kuwa mashindano hayo yaliandaliwa kwa ajili ya wachezaji wa kulipwa na wa ridhaa, lakini pia wakaamua kuwaingiza wachezaji wasindikizaji ili kukuza vipaji vya chipukizi katika mchezo huo.
Naye mcheza gofu Christina Charles alisisitiza kuwa ushindi katika mchezo huo unahitaji nidhamu, mazoezi ya mara kwa mara, pamoja na kujituma kwa hali ya juu.