
Dar es Salaam, Ubongo, shirika linaloongoza Afrika katika kutoa elimu burudani linayo furaha kutangaza uzinduzi wa msimu wa tano wa kipindi chake cha maendeleo ya awali kwa watoto, Akili and Me, kikiwa na mwonekano mpya wa kuvutia na dhamira ya kuwasaidia watoto wadogo kuelewa hisia zao, kujenga ustahimilivu na kukuza uelewa.
Kupitia muziki, simulizi, na vipindi shirikishi, msimu huu mpya unainua kiwango cha kupata mafunzo ya awali kwa kuweka mkazo mkubwa kwenye Elimu ya Kijamii na Kihisia (SEL), ukiwapa watoto nyenzo za kutambua na kueleza hisia zao vizuri.
“Kwa msimu wa tano, tulitaka kuongeza wigo wa mafunzo ya awali ya mtoto kiakili na kuzingatia jambo la msingi la kuwasaidia watoto kuelewa na kuelezea hisia zao,” alisema Tamala Maerere-Kateka, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano ya Kimkakati katika shirika la Ubongo.,” alisema Tamala Maerere-Kateka, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano ya Kimkakati katika shirika la Ubongo.
“Tunaamini kuwa watoto wanapojifunza jinsi ya kueleza na kushughulikia hisia zao, wanajenga kujiamini na uthabiti wanaohitaji ili kustawi shuleni na maishani.”
Msimu huu mpya umeboreshwa kwa kutumia mbinu za kisasa za uhaishaji (animation) kuleta mvuto zaidi kwa watazamaji.
Ubongo pia umeongeza wigo wa mafunzo kwa kuzindua Michezo ya Akili and Me kupitia programu ya Ubongo Playroom—kipengele shirikishi kilichobuniwa kuongeza ushiriki wa watoto wa kujifunza kupitia michezo. Programu hii inajumuisha video za kielimu, hadithi za sauti, vitabu pepe, na michezo, hivyo kumpa mtoto uzoefu wa kujifunza uliokamilika na wa kufurahisha. Inaweza kupakuliwa kupitia Google Play na App store.
“Tunajua watoto hujifunza vizuri zaidi kupitia michezo,” alisema Maerere-Kateka. “Kwa kuongeza vipengele vya ushiriki, tunawapa watoto nafasi ya kuchukua umiliki wa mchakato wao wa kujifunza.”
Kupitia msimu wa tano, Ubongo inaendeleza dhamira yake ya kufanya mafunzo ya awali kuwa yenye athari chanya kwa watoto barani Afrika.
“Hisia kubwa zinaweza kuwa ngumu kwa watoto wadogo kuelezea, lakini wanapokuwa na maneno na nyenzo za kujieleza, wanapata ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha,” alisema Maerere-Kateka.