NA DENIS MLOWE IRINGA
WALIOKUWA wabunge wa viti Maalum Mkoa wa Iringa, Rose Tweve na Nancy Nyalusi wamefanikiwa kuibuka kiddedea Katika uchaguzi wa Ubunge viti maalum Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoa wa Iringa,
Rose Tweve ameibuka kinara kati ya wagombea 8 akipata kura za wajumbe 594 akifuatiwa na Nancy Nyalusi akipata kura 507, huku nafasi ya tatu akipata aliyetegemewa na wengi kuibuka mshindi injinia Fatma Rembo aliyepata kura 326.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo Kheri James ambaye ni mkuu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa wagombea wengine ni Seki Kasuga aliyepata kura 152 Tumaini Msowoya kura 31 Scola Mbosa kura 8 Maria Makombe kura 59 na Lydia Nzema. kura 25.
Akizungumza mara baada ya kutangaza matokeo hayo katika Uchaguzi huo ulifanyika katika ukumbi wa Masiti Hall, uliopo Kata ya Gangilonga, Manispaa ya Iringa, mkuu wa mkoa Kheri James alisema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 852, huku kura 851 zikihesabiwa kuwa halali na kura moja ikiharibika.
Kheri James amewapongeza wagombea wote kwa kuendesha kampeni za kistaarabu na kuonesha mshikamano mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Aidha, aliwapongeza wajumbe kwa kushiriki kwa umakini na kufuata taratibu zilizowekwa, jambo ambalo liliwezesha uchaguzi kufanyika kwa mafanikio na kwa utulivu.
Mara baada ya kutangazwa kuongoza kura za maoni Rose Tweve aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kumpa imani tena ya kuwawakiridha na kuendelea kumwombea kwa Mungu kwani ndio kwanza kazi imeanza hadi pale chama kitakapomuidhinisha kuwa mbunge rasmi.
Alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kusimamia uchaguzi kwa uhuru na hadi na kuwashukuru wagombea wenzake kwa wote kwa kuweza kujitokeza katika kuwania nafasi hiyo.
Naye Nancy Nyalusi aliwashukuru wajumbe na viongozi wa Ngazi za Juu kurudisha jina lake mwisho kupata nafasi ya kuwawakilisha wanawake kwa miaka 5 mingine.
Wabunge hao watarajiwa wakati wote walikuwa wakilia mara baada ya matokeo kutangazwa kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo awali kutoka kwa wagombea wengine mjini hapa.