Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Afisa Mipango kutoka Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Bi. Eva Msangi, amesema kuwa moja ya faida kubwa ya Soko hilo ni kuchangia ongezeko la fedha za kigeni nchini kupitia minada ya bidhaa na usafirishaji wake kwenda nje ya nchi.
Akizungumza leo, Agosti 3, 2025, katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, Bi. Msangi alisema bidhaa zinazouzwa kupitia soko hilo ni pamoja na kahawa, korosho, kokoa, ufuta, dengu na mbaazi.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25 bidhaa zilizouzwa kupitia minada ya TMX zimefikia tani 90,928 zenye thamani ya Shilingi bilioni 256.6,” alisema Bi. Msangi na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kichocheo kikubwa cha ongezeko la fedha za kigeni nchini.
Aidha, aliwahimiza wananchi na wadau wa biashara kutembelea Banda la TMX lililopo katika viwanja vya maonesho hayo ili kujionea bidhaa zinazouzwa na kupata elimu kuhusu namna Soko la Bidhaa Tanzania linavyofanya kazi.