FARIDA MANGUBE,MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amewataka wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kutumia kikamilifu fursa ya uwepo wa maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi maarufu kama Nanenane kujifunza teknolojia bunifu zinazotolewa na taasisi mbalimbali, ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ili waweze kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zao.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la TFS kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro, Dkt. Buriani aliipongeza TFS kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda misitu, kuhifadhi mazingira na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali misitu.
“Nawapongeza sana TFS kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa misitu yetu na kwa jitihada kubwa wanazozifanya kufikisha elimu kwa wananchi kupitia maonesho haya. Ni muhimu wananchi hasa wakulima na wafugaji kutembelea banda la TFS ili kujionea teknolojia mbalimbali wanazotumia, kupata elimu kuhusu namna bora ya kuhifadhi mazingira, na hasa namna ya kujikinga dhidi ya moto mwitu ambao umekuwa tishio kwa misitu yetu,” alisema Dkt. Buriani.
Kwa upande wake, Mhifadhi mkuu ugani na uenezi TFS Kanda ya Mashariki Shabani Kiulah, alisema kuwa TFS imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi salama ya moto hasa wakati wa kuandaa mashamba ili kuepusha athari za moto mwitu kwa mazingira na misitu ya asili.
“Katika maonesho haya tunawapa wananchi mbinu na teknolojia za kisasa za uhifadhi na usimamizi wa misitu, ikiwa ni pamoja na njia sahihi za kuzima moto na jinsi ya kutumia moto kwa usalama bila kuharibu mazingira. Tunawahimiza wananchi watembelee banda letu ili wajifunze zaidi na washiriki katika juhudi za kitaifa za kuhifadhi rasilimali za misitu,” alisema Kiulah.
Aidha, Kiulah alisisitiza kuwa elimu inayotolewa na TFS si tu kwa wakulima na wafugaji, bali pia kwa wanafunzi na vijana wanaotembelea banda hilo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha kizazi kijacho kujali na kulinda mazingira.
Maonesho hayo ya mwaka huu 2025 yanabeba kaulimbiu: “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”, na yanajumuisha washiriki kutoka mikoa minne ya Kanda ya Mashariki ambayo ni Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.