Na Mwaandishi Wetu Lindi
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI), kituo Cha Naliendele Mkoani Mtwara kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Nchini (CBT) kwa mara nyingine wamendaa siku maalumu ya kuhamasisha ulaji na unywaji wa bidhaa zinazotokana na zao la korosho ili kuongeza soko la ndani.
Shughuli hiyo ambayo pia imelenga pia kuongeza juhudi za kuchakata zao la korosho hapa nchini imeandaliwa katika maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini Mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ilifanyika jana (Agosti 5l), mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Michael Mtenjele amesema hatua hiyo itasaidia kulinda soko la korosho nchini.
“Napongeza sana TARI Naliendele na Bodi yetu ya korosho kwa hatua hii ya kuhamasisha ulaji na unywaji wa bidhaa za korosho, itasaidia kuongeza soko la ndani lakin pia kulinda soko la korosho nchini na kupunguza uhitaji wa kupata masoko nje,” amesema.
Mtafiti wa Zao la Korosho kutoka TARI Naliendele Dkt Wilson Nene amesema hafla ya ulaji na unywaji wa bidhaa za korosho umelenga kutangaza uzuri wa bidhaa ndani na nje ya Tanzania.
Kaimu Mkurungezi Mkuu wa CBT Magire Maregesi amesema siku ya ulaji wa na unywaji wa bidhaa za korosho umelenga kuongeza kuhamasisha watanzania kula vyakula vya Korosho kujenga afya, uchumi nchini na kumuongezea mkulima kipato aone umuhimu wa kuongeza uzalishaji.
“Serikali imeweka msisitzo mkubwa sana kwenye zao la korosho kuhakikisha kwamba linatuzika ndani na nje ambapo nje tunapata fedha nyingi za kigeni,” amesema na kuongeza kuwa ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, imeanzisha viwanda vya kubagua na kuchakata bidhaa mbalimbali za zao la korosho Mkoani Mtwara.
“Lakini pia imeongeza kwa ukubwa sana utoaji wa pembejeo, wataalamu wakiwemo maafisa ugani kusaidia wakulima kuzalisha kwa tija,” amesema.
Baadhi ya bidhaa za korosho zilizoandaliwa ni korosho za kula zenye ladha mbalimbali, maziwa ya korosho, maziwa yenye ladha ya strawberry na chocolate, mandazi.