Na Alex Sonna,Dodoma
KAMISHNA wa Maadili, Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi, amesema Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uadilifu, akisisitiza kuwa maadili mema ndiyo nguzo ya msingi ya maendeleo ya jamii yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 6,2025 katika banda la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Kamishna Mwangesi amesema uadilifu ni tabia ya kufanya matendo mema bila kuumiza wengine au kudhulumu haki za watu, jambo ambalo huimarisha mshikamano na ustawi wa kijamii.
“Jamii yenye uadilifu hujengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, kutimiza wajibu, na kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo,” amesema Kamishna Mwangesi
Aidha, Kamishna Mwangesi ametoa wito kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025, kuchagua viongozi waadilifu watakaoweka mbele maslahi ya umma kuliko maslahi binafsi.
“Viongozi waadilifu hawatumii nafasi zao kujinufaisha, bali huhakikisha huduma za jamii zinatolewa kwa haki, mali za umma zinasimamiwa kwa uwajibikaji, na wananchi wote wananufaika,” ameongeza.
Amesema kuwa kiongozi mwenye maadili hujenga imani kwa wananchi, hudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuchochea maendeleo endelevu kupitia sera jumuishi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuanza kuwafundisha watoto na vijana maadili mema wakiwa bado shuleni na majumbani, kwa lengo la kuandaa kizazi chenye uadilifu na uwezo wa kulinda rasilimali za taifa.
Kamishna Mwangesi ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kusambaza elimu ya maadili, ili kuimarisha misingi ya uwajibikaji na uadilifu kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.


