
Asema aliimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali
Atoa rai kwa Watanzania kuenzi mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 11, 2025 amemwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Yustino Ndugai, yaliyofanyika shambani kwake, kijiji cha Msunjulile, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Akizungumza katika ibada ya mazishi, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuenzi mema yote yaliyofanywa na Hayati Ndugai enzi za uhai wake, akisema mchango wake katika uongozi wa Bunge na Taifa kwa ujumla utabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo.
Amesema kuwa akiwa mwakilishi wa wananchi wa Kongwa, hayati Ndugai ametoa mchango mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake, na kwamba wote ni mashuhuda wa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii. “Serikali itaendelea kumuenzi kwa yale yote aliyoyafanya kwa wanaKongwa”
Aidha, Waziri Mkuu ameeleza kuwa hayati Ndugai alikuwa mlinzi wa taratibu za Bunge na mshirika wa karibu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa, akisisitiza mawasiliano ya uwazi, mshikamano na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa ajenda za kitaifa.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amemtaja hayati Ndugai kama kiongozi mwenye weledi, uadilifu, unyenyekevu, na mchapakazi ambaye alibeba heshima ya mkoa wa Dodoma na jimbo la Kongwa kupitia uongozi na siasa za uwajibikaji.
Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itasimamia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ya kukamilishwa kwa masuala yote yaliyoanzishwa na Hayati Ndugai, pamoja na kuendeleza makumbusho ya Kongwa ikiwa ni kielelezo cha kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa afrika. “Tutasimamia agizo hili kwa ukamilifu.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Kongwa na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na msiba wa hayati Ndugai.
Naye, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa wanaamini katika kumuenzi hayati Ndugai na watamkumbuka daima kwa kuendeleza misingi pamoja na mambo mema yote aliyoyatenda wakati wa uhai wake.
Mazishi ya Hayati Ndugai yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena Saidi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, viongozi wengine kitaifa, ndugu, jamaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Hayati Job Ndugai alifariki agosti 06, 2025 jijini Dodoma kwa Shinikizo la damu lililoshuka sana