
Kocha mpya wa Tottenham Hotspur, Thomas Frank, amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mtanange wa UEFA Super Cup Jumatano dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain. Spurs, wanaoshiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hii, walimaliza ukame wa miaka 17 bila taji baada ya kutwaa Europa League mwezi Mei chini ya Ange Postecoglou
Licha ya mafanikio hayo alifutwa kazi mapema mwaka huu kutokana na matokeo mabovu ya ligi. Frank sasa anakabiliwa na changamoto ya kuwakosa wachezaji muhimu kama James Maddison na Yves Bissouma, huku mshambuliaji nyota Son Heung-min akiaga klabu.

PSG, chini ya kocha Luis Enrique, wanaingia kwenye mchezo huu bila maandalizi ya kawaida baada ya kushiriki Kombe la Dunia la Klabu ambapo walipoteza 3-0 dhidi ya Chelsea. Timu hiyo ilimaliza msimu uliopita kwa mataji matatu—Ligue 1, Coupe de France, na taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa kihistoria wa 5-0 dhidi ya Inter Milan.
Hata hivyo, habari kubwa kambini mwao ni kuachwa kwa kipa wao nyota Gianluigi Donnarumma kwenye kikosi cha fainali, jambo lililozua mjadala mkubwa kabla ya pambano.
Enrique anakiri kukosa maandalizi bora kunaweza kuwa changamoto, lakini anasema ari ya kuandika historia zaidi ndiyo itakayowasukuma wachezaji wake.
Kwa Frank, fainali hii ni nafasi ya kuonyesha mwelekeo mpya wa Spurs na kujijengea heshima dhidi ya wapinzani wakubwa wa bara Ulaya. “Hii ni mechi ya kuonyesha umoja, nidhamu na ushindani wa hali ya juu,” amesema Frank, akiongeza kuwa katika mchezo mmoja, Spurs wana nafasi sawa ya kushinda kama PSG.