Kibaha, 13 Agosti 2025,
Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa mafunzo maalum kwa Watendaji wa Elimu ngazi ya Halmashauri, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na walimu wa Taaluma wa Sekondari pamoja na maafisa kutoka ofisi za Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya na Wathibiti Ubora wa Shule Wilaya.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo washiriki juu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 (Mtaala Mpya Ulioboreshwa) pamoja na utaratibu na mfumo mzima wa utahini. Mafunzo hayo yaliendeshwa na wataalamu kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Taasisi Binafsi ya Educate!
Mafunzo hayo yameandaliwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Jacob Shemwelekwa ikiwa ni sehemu ya juhudi na jitihada za Halmashauri kuwajengea uwezo watendaji na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ili kufikia lengo la Serikali la mabadiliko ya kweli katika Elimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo , Mwalimu Isihaka Rashid, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kibaha akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha alisema kuwa mabadiliko ya mtaala ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha elimu na kuendana na mahitaji ya sasa katika nyanja zote za kielimu, kijamii, mabadiliko ya kiuchumi na sokonla ajira la dunia. Amewataka washiriki kuhakikisha wanatumia maarifa watakayayopata katika kuimarisha ufundishaji, ujifunzaji na uendeshaji wa shule.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta ufanisi zaidi katika kusimamia elimu katika Manispaa ya Kibaha na kuhakikisha kuwa wanafunzi kwa kusaidiana na walimu na wazazi wanachagua kwa usahihi mkondo wa jumla au amali kulingana malengo kusudiwa.
Aidha, mara baada ya mafunzo washiriki walikiri kupata uelewa wa kutosha juu ya Mtaala Ulioboreshwa na kuahidi kuboresha utoaji wa elimu kwa mfumo mpya ili kuendana na malengo ya Serikali, wanafunzi na jamii kwa ujumla. Walimu wanaamini kuwa elimu na maarifa waliyoyapata yataleta mabadiliko chanja katika ufundishaji, ujifunzaji na utahini wa watahiwa.
Katika hatua nyingine shule zote za sekondari za Serikali za Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha zipatazo 24 na shule za sekondari zisizo za Serikali 6 zimeahidi kuanza kutoa mafunzo ya amali ya fani mbalimbali mwaka mpya wa masomo ifikapo Januari 2026.
Wakati wa ufungaji wa Mafunzo hayo, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mwalimu Rashid aliwasihi washiriki kutoa mafunzo ya elimu hiyo kwa walimu, wazazi na wanafunzi ili wote wapate uelewa wa kutosha na kurahisisha utoaji wa elimu na malengo yaliyokusudiwa. Mwisho alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Shemwelekwa kwa maono yake mazuri ya utoaji wa mafunzo hayo kwa viongozi na walimu kwa ngazi ya sekondari.