Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo amesema kuwa licha ya changamoto za kisiasa, uhalifu unaovuka mipaka na matatizo ya kiuchumi kwa jamii ambayo yanaendelea kutafutiwa ufumbuzi, bado Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimepiga hatua kubwa katika kuimarisha amani na utulivu, mshikamano na utawala bora.
Ameyasema hayo wakati anafungua Mkutano wa Utatu wa Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama jijini Antananarivo, Madagascar Agosti 15, 2025.
“Licha ya changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi wanachama na ulimwengu kwa ujumla, eneo letu limebaki kuwa himilivu, likiendelea kutekeleza majukumu yake kwa ajili ya kuyafikia malengo ya kisiasa na kiuchumi kwa manufaa ya watu wetu”, Balozi Shelukindo alisema.
Balozi Shelukindo amesema ni jambo lisilopingika kwamba amani na utulivu ni msingi wa kuyafikia maendeleo endelevu, hivyo, alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kufanya kila linalowezekana ili eneo hilo liendelee kubaki kuwa tulivu wakati wote.
Alisema ili lengo hilo liweze kutimia, alihimiza nchi wanachama kulipa kipaumbele kwa kujijengea uwezo katika kuhamasisha jitihada za kuzuia migogoro, usuluhishi wa migogoro, kujenga na kulinda amani.
Allhitimisha hotuba yake kwa kuzitakia kheri nchi wanachama zinazojiandaa na uchaguzi mkuu ambazo ni Malawi, Ushelisheli na nchi yake Tanzania. Alisema Tanzania inasubiri kwa hamu kubwa kupokea timu ya waangalizi ya SADC ambapo maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025 yanaendelea.