
Watafiti wametangaza uvumbuzi wa aina mbili za dawa mpya za kupambana na maambukizi sugu (antibiotics) zinazoweza kuua vimelea vya kisonono sugu na MRSA.
Dawa hizo, zilizotengenezwa na Akili Mnemba kwa kutumia chembe ndogo sana, zimeonyesha uwezo wa kuua bakteria hao katika majaribio ya maabara yaliyohusisha wanyama.
Ingawa michanganyiko hii miwili bado inahitaji miaka ya uboreshaji na majaribio ya kimatibabu kabla ya kutumika kwa wagonjwa, timu ya Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) inasema uvumbuzi huu unaweza kuanza “enzi mpya ya dhahabu” katika ugunduzi wa dawa za kuua bakteria.
Hii ni hatua muhimu kwani maambukizi sugu sasa yanasababisha vifo vya zaidi ya milioni moja kila mwaka. Matumizi kupita kiasi ya dawa za bakteria yamesababisha bakteria kubadilika ili kuepuka athari za dawa, huku uhaba wa dawa mpya unaendelea kwa miongo kadhaa.