
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekosoa vikali hatua ya Kenya kuteua afisa wake wa kidiplomasia katika mji wa Goma, ulioko mashariki mwa Congo na kwa sasa ukidhibitiwa na waasi wa kundi la M23.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Congo, uteuzi huo unaweza kuonekana kama hatua ya kuhalalisha kile ilichoeleza kuwa ni “ukaliaji kinyume cha sheria wa eneo la taifa” na kundi la waasi.
Orodha ya uteuzi wa wanadiplomasia iliyotangazwa na Rais wa Kenya, William Ruto, ilihusisha mabalozi wapya nchini Ethiopia, Saudi Arabia na Kamishna Mkuu wa Uingereza, pamoja na nafasi ya kidiplomasia katika mji wa Goma. Ingawa nafasi hiyo si mpya, muda wa tangazo hilo ndio uliosababisha hasira upande wa Kinshasa.
DRC ilipoteza udhibiti wa Goma pamoja na maeneo mengine yenye utajiri wa madini mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuzingatiwa na waasi wa M23. Hali hiyo imeendeleza mvutano mkubwa katika ukanda huo, ambapo licha ya pande husika kuahidi kusitisha mapigano, makabiliano yameendelea kushuhudiwa