Mnamo mwezi Machi mwaka jana wakati Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) iliposaini mkataba wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kahama-Bulyanhulu JCT- Kakola yenye kilomita 73 na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ufadhili wa Barrick wa gharama ya shilingi bilioni 101.2 , ilikuwa ni faraja kubwa kwa watumiaji wengi wa barabara hiyo ambayo ilikuwa ni moja ya kero kubwa ya muda mrefu kutokana na kuwa katika hali mbaya wakati wote iwe kipindi cha mvua ama kipindi cha kiangazi.
Wananchi waliona kuwa sasa wakati wao wa kujikwamua kiuchumi umewadia, kwa kuwa ujenzi huo ukikamilika utazidi kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.
Kilichofurahisha zaidi ni kuona ujenzi huo unafadhiliwa na migodi ya Barrick nchini ambayo inaendeshwa kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corporation. Migodi hiyo ni Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa.
Kutekelezwa kwa mradi huu mkubwa unaofadhiliwa na mwekezaji mkubwa nchini katika sekta ya madini, ni moja ya kielelezo kinachodhihirisha kuwa Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inaweza kufanya mambo makubwa mojawapo ikiwa ni ujenzi wa miundombinu bora ya barabara,reli na mingineyo ambayo ni moja ya kichocheo cha ukuaji uchumi katika taifa na kufanya maisha ya wananchi kuwa mazuri.
Pia mradi huu unadhihirisha kuwa usimamizi wa rasilimali ya madini na nyinginezo nchini ukipata wawekezaji wazuri na kusimamiwa ipasavyo unaweza kuleta maendeleo makubwa nchini kwa haraka.
Kama kampuni moja imeweza kutoa kiasi cha shilingi bilioni 101.2 kujenga kipande kikubwa kama hiki cha barabara kwa kiwango cha lami tafsiri yake ni kwamba ukiwa na wawekezaji wakubwa wapatao hata 100 kwa idadi wakawekewa mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuwekewa sheria na sera rafiki zisizobadilika kila wakati na kusimamiwa ipasavyo wanaweza kutoa mchango mkubwa wa fedha za kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo .
Mpaka sasa kasi ya mradi huu unaojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa kusimamiwa na kitengo maalumu cha ushauri wa Kihandisi ndani ya Wakala ya Barabara Tanzania-TANROADS (Tanroads Engineering Consulting Unit-TECU) unaendelea vizuri na madaraja katika baadhi ya maeneo korofi yanaendelea kujengwa.
Waziri wa Ujenzi wa wakati huo,Innocent Bashungwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wa barabara hii uliofanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alisema barabara hiyo imekuwa moja ya kero kubwa kwa wananchi kwa muda mrefu na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameipatia suluhisho kwa ushirikiano mzuri na wawekezaji wa ndani ya nchi ikiwemo kampuni ya Barrick na kutoa kibali barabara hiyo iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Kwa niaba ya Serikali,Waziri Bashungwa aliishukuru kampuni ya Barrick kwa kufadhili mradi huu mkubwa wa kilometa 73 na kuahidi kuwa kwa mujibu wa mkataba ujenzi wa barabara hii utatekelezwa ndani ya miezi 27 kwa maana ya kwamba utakamilika mwaka wa 2027.
Hivi karibuni Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Samwel Mwambungu,alikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kukaririwa na vyombo vya habari ekieleza kuwa ujenzi unaendelea vizuri na kuielezea barabara hiyo kuwa ni fursa ya kufungua milango ya kiuchumi nchini na inafungua milango kwa wawekezaji na wafanyabiashara wazawa pia ni moja ya mikakati ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.
Mradi huu pia umeleta faraja kwa wananchi mbalimbali ambao wameajiriwa kufanya kazi mbalimbali katika mchakato huu wa ujenzi na wanaendelea kujipatia kipato sambamba na wafanyabiashara katika eneo inapopita barabara wameanza kunufaika kwa biashara zao kuchangamka kutokana na kuongezeka kwa watu.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo na watumiaji wa mara kwa mara wa barabara hii inayoendelea kujengwa walipohojiwa wiki hii, walisema barabara ilikuwa katika hali mbaya na kuwasababishia usumbufu mkubwa na hasara na walitoa shukrani kwa Serikali na kampuni ya Barrick kwa kuijenga tena kwa kiwango cha lami.
Akiongea kwa niaba ya Wananchi wenzake, Mwandu John, mkazi wa kijiji cha Ntobo kilichopo Halmashauri ya Msalala, alisema barabara hiyo ilikuwa na mashimo makubwa ambayo yamekuwa yakisababisha kuharibika kwa vyombo vya usafiri na kuongeza gharama za maisha kutokana na kupoteza muda mwingi kutoka Kahama mpaka Bulyanhulu wakati kupande hicho kama barabara ni nzuri ni kifupi.
“Tunayo furaha kubwa kuona barabara hii inatengenezwa kwa kuwa mbali na kurahisisha maisha itaaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo haya yaliyokuwa yanafifishwa na ubovu wa miundombinu.Tunashukuru Barrick kwa kuendelea kudhihiriha kuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika mkoa huu” alisema Mwandu John kwa furaha akiungwa mkono na wenzake.
Naye Samwel Petro akiongea kwa niaba ya madereva wa vyombo vya moto wanaotumia barabara hiyo alisema kwa muda mrefu ubovu wa barabara unawasababishia hasara kubwa ya kuharibika kwa vyombo vyao,anaamini sasa ujenzi ukikamilika tatizo hilo litaisha na fursa za biashara zinaongezeka sambamba na wananchi wengi kuweza kujiajiri na kuboresha maisha yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa mrejesho wa mkakati wake endelevu wa miaka sita wa kampuni ya Barrick Mining Corporation akiwa nchini Canada hivi karibuni, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu, Mark Bristow, alisema kampuni inaendelea kuendeleza miradi ya ukuaji wa msingi iliyoundwa kuleta thamani ya muda mrefu kwa wadau wote kupitia ushirikiano wa kweli.
Alisema vipaumbele vya uendelevu vya Barrick ni pamoja na utekelezaji Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), kudumisha dhamira yake isiyoyumba ya usalama mahali pa kazi, na kuchukua tahadhari za matukio ya mbele na udhibiti wa uchafuzi wa hali ya hewa kutokana na shughuli zake.
“Mkakati wetu wa uendelevu sio tu mfumo – ni jinsi tunavyounda athari za kudumu, zinazowajibika,”alisema Rais wa Barrick na Afisa Mtendaji Mkuu Mark Bristow na kuongeza “Uchimbaji madini ukifanyika kwa umahiri ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo. Jamii zinazoishi kwenye maeneo ya shughuli zetu zikipata mafanikio ni mafanikio kwetu pia .”