*Wananchi watakiwa kuitunza miundombinu hiyo
Mara.
Jumla ya shilingi Milioni 148.5 zimetumika Kujenga Daraja la kinyang’erere lililopo katika kijiji cha kinyang’erere halmashauri ya Musoma Mkoani Mara.
Akisoma Taarifa ya ujenzi wa Mradi huo Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Musoma Mhandisi Mohmed Etanga amesema daraja hilo limekamilika ujenzi wake kwa asilimia mia moja na kutoa huduma kwa Wananchi kama ilivyo kusudiwa.
Mhandisi Etanga ameongeza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa kijiji hicho kwaajili ya usafirishaji wa Mazao na kwenda kupata huduma za kijamii katika vijiji vingine ambapo kuna kituo cha Afya pamoja na wanafunzi kuvuka kwenda shule.
Ameongeza kuwa kipindi cha Masika wakazi hao walikuwa wakipitia kadhia ya kushindwa kuvuka mto ambao unakuwa umejaa maji jambo lilikuwa likisababisha baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani na kushindwa kuuza mazao yao kutokana na ubovu wa barabara .
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi ameipongeza TARURA kwa kufanya kazi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa.
” Nichukue nafasi hii kumpongeza Meneja wa TARURA Mkoa na timu yake kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa “amesema Ussi.
Mbali na kutoa kongole kwa watumishi wa TARURA amemshukuru pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa Fedha nyingi kwa lengo la Ujenzi wa Miradi ya maendeleo kwa wanachi katika maneno mbalimbali nchini.
Mbali na hilo Ussi amewaasa wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iwe endelevu kutokana na kutumia gharama nyingi katika utengenezaji wake na endapo wataitunza itaendelea kuwa imara na kutumika kwa kipindi kirefu zaidi.