
Mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Qashi, Yohana Amani Konki (18), umepumzishwa Agosti 19, 2025, katika kijiji cha Samas, wilayani Babati mkoani Manyara, siku tatu baada ya kifo chake kilichotokana na kushambuliwa na wanafunzi wenzake kwa tuhuma za wizi wa simu.
Mwanafunzi huyo alifariki dunia alfajiri ya Agosti 16, 2025, baada ya kudaiwa kuhusishwa na wizi wa simu kufuatia ramli ya mganga wa kienyeji, hali iliyochochea wenzake kumvamia na kumjeruhi vibaya hadi kupoteza maisha.
Mazishi yake yamehudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wa kijiji, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi na kuwashikilia wanafunzi 11 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.