Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyamapori TAWA kutoka Mpanga Kipengele linamshikilia Frank Alon mwenye umri wa miaka 49 mkazi wa Uyole Nsalaga jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali ambapo alikamatwa akiwa na meno nane ya tembo yenye uzito wa kilo 31.6 bila kibali Tukio hilo lilitokea Agosti 17 mwaka 2025 majira ya saa 9:00 alasiri katika kijiji cha Nsonyanga kata ya Mahongole tarafa ya Ilongo wilaya ya Mbarali ambapo mtuhumiwa huyo alikamatwa wakati wa misako na doria za pamoja akitumia pikipiki yenye namba za usajili MC 165 DDF aina ya TVS kusafirisha meno hayo huku akitafuta mteja Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni mwindaji haramu anayejihusisha na ujangiri ndani ya hifadhi za taifa
Katika tukio jingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la Umeme TANESCO Tawi la Mbeya linamshikilia Ikupa Mwakibibi mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni mjasilimali na mkazi wa Sae jijini Mbeya kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya shirika hilo kwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria Mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 18 mwaka 2025 majira ya saa 9:30 alasiri katika mtaa wa Sae kata ya Ilomba ambapo baada ya upekuzi alikutwa akiwa na mita 19 za umeme rimoti 45 za TANESCO pamoja na rola 25 za waya vyote vikiwa mali ya shirika hilo
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na WhatsApp Watuhumiwa wanne walikamatwa Agosti 18 mwaka 2025 saa 6:00 mchana katika kitongoji cha Nsalala tarafa ya Usongwe ambapo walikuwa wakitumia mbinu za kutengeneza link ghushi za ajira kwenye supermarket iitwayo Kajala jijini Dar es Salaam na kuwatapeli waombaji ajira kwa kuwataka watume fedha za kulipia fomu na sare Watuhumiwa hao ni Nemia Japhet Njonga mwenye umri wa miaka 23 fundi rangi mkazi wa Mwakapangala Ombeni Asangalwisye Ambilikile mwenye miaka 22 bodaboda mkazi wa Nsalala Jacob Peter Hamis mwenye miaka 23 fundi rangi mkazi wa Mwakapangala pamoja na Baraka Joniphat Mgala mwenye miaka 22 bodaboda mkazi wa Ndola Mbalizi Baada ya upekuzi walikutwa na simu na laini za mitandao tofauti zilizokuwa zikitumika kwa mawasiliano na kupokelea fedha
Katika mtaa wa Mapelele kata ya Nsalala polisi waliwakamata watuhumiwa wengine watatu kwa tuhuma kama hizo ambao ni Lusajo Jeremiah mwenye miaka 45 mkazi wa Ndola Mbalizi Adili Mbeyale mwenye miaka 19 mkazi wa Ndola Mbalizi pamoja na Shaban Yasin Thabiti mwenye miaka 23 mkazi wa Mshikamano ambapo walikutwa na simu ndogo aina ya Itel tatu Tecno mbili na laini 20 walizokuwa wakizitumia kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kwa kudai wanauza bidhaa kwa bei nafuu
Aidha Jeshi la Polisi limewakamata Ester Kimaro mwenye miaka 28 mfanyabiashara na mkazi wa Nzovwe pamoja na Abdi Awadhi mwenye miaka 21 mkazi wa Iyunga kwa tuhuma za kuwarubuni wananchi kupitia kampuni inayojulikana kama Q Net yenye makao yake Malaysia na kuchangisha fedha ili watu wawe wamiliki wenza wa kampuni hiyo Katika tukio hilo lililofanyika Agosti 18 mwaka 2025 mtaa wa Ndanyela kata ya Nzovwe walikutwa watu 27 wakiwemo wanawake 8 na wanaume 19 wakiendelea na zoezi la kuchangishana fedha kwa ajili ya kutumwa Q Net ambapo uchunguzi umebaini kuwa jumla ya shilingi milioni 44 laki nne na elfu thelathini na tano zilichangishwa kutoka kwao
Katika muendelezo wa misako hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata watuhumiwa wengine kwa tuhuma za kupatikana na pombe haramu na dawa za kulevya ambapo Agripa Godwini mwenye miaka 27 mkazi wa Mikumi na Kaiza Mwandambo mwenye miaka 54 mkazi wa Kukisya wilayani Kyela walikamatwa wakiwa na pombe haramu aina ya gongo ujazo wa lita 150 wakiwa wanazisafirisha kwa kutumia pikipiki yenye namba MC 528 ESM aina ya Boxer Vilevile Patrick Chamugwana mwenye miaka 48 dereva na mkazi wa Majani Mapana mkoani Tanga alikamatwa Agosti 19 mwaka 2025 saa 11:00 jioni akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi zenye uzito wa kilo 10 alizokuwa akizisafirisha kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam kwa kutumia basi la abiria la Achimwene lenye namba T 949 EGD aina ya Yutong ambapo alizificha kwenye begi jeusi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya ujangiri uhalifu na utapeli na badala yake wajihusishe na kazi halali zitakazowaingizia kipato sambamba na kusisitiza umakini katika matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka kudanganywa na matapeli wanaotumia teknolojia hiyo vibaya kwa malengo ya kujipatia fedha.