

Putin agoma kukutanishwa na Zelensicky Ikulu ya Urusi imepuuzilia mbali mazungumzo ya kufanyika kwa mkutano kati ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, licha ya wito uliotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, akihimiza viongozi hao kukutana ili kujadili kumaliza vita nchini Ukraine.
Shinikizo la kufanyika kwa mazungumzo hayo linakuja baada ya Trump kukutana na Putin mjini Alaska wiki iliyopita, na kisha kuwakaribisha viongozi saba wa Ulaya pamoja na Zelensky katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu.

Trump alikiri mzozo huo ni “vigumu” kusuluhisha, huku akionya kuwa huenda Rais Putin hakutaka kumaliza uhasama. “Tutajua kuhusu Rais Putin katika wiki kadhaa zijazo. Inawezekana kwamba hataki kufanya makubaliano,” alisema Jumanne. Aidha, aliongeza kuwa Putin anapitia “wakati mgumu” bila kutoa maelezo zaidi.
Siku ya Jumatatu, Putin alimwambia Trump kuwa yuko “sawa” na wazo la mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine, lakini siku iliyofuata Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alilitupilia mbali pendekezo hilo, akisisitiza kuwa mkutano wowote lazima utayarishwe hatua kwa hatua kuanzia ngazi ya wataalam.

Dmitry Polyanskiy, Naibu Mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, alikiambia chombo cha habari cha BBC kuwa “hakuna mtu aliyekataa” uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja, lakini akaonya kuwa “haipaswi kuwa mkutano kwa ajili tu ya mkutano uwe umefanyika.”
Wakati huo huo, taarifa zilidai kwamba Putin alipendekeza kwa Trump kuwa Zelensky asafiri hadi Moscow kwa mazungumzo, pendekezo ambalo Ukraine ilikataa mara moja. Wachambuzi wanasema hatua hiyo inaweza kuwa mbinu ya Urusi kuweka sharti lisilowezekana ambalo Ukraine haiwezi kulikubali.