……….
Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Agosti 20, 2025, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyegezi, ambacho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 270 hadi kukamilika kwake.
Mtanda alisema kuwa kituo hicho kimepata msukumo wa kukamilika kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, ambapo kituo hicho kitazinduliwa rasmi na kuanza kutumika tarehe 25 Agosti 2025.
“Tuliona kuwa ili Kituo hiki kikamilike ni lazima kiwe kwenye mradi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru. Tusipokiweka kwenye mradi huo, hakitakamilika kwa haraka,” alisema Mtanda.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Afisa Mnadhimu Namba Moja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Gideon Msuya alisema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu na lipo tayari kuwatumikia wananchi kwa weledi na kwa kuzingatia haki.
“Kama ilivyo ada, kazi yetu ni kulinda raia na mali zao. Tupo tayari kuwatumikia wananchi. Tunachoomba kutoka kwao ni ushirikiano,” alisema SACP Msuya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alisema ujenzi wa kituo hicho ni jitihada za Jeshi la Polisi kusogeza huduma karibu na wananchi, jambo litakalosaidia kupunguza kero za kiusalama katika eneo hilo.
“Polisi wanaposogeza huduma karibu na wananchi haimaanishi huduma hiyo ilikuwa mbali, bali ni juhudi za Jeshi la Polisi. Kwa hili, nalipongeza sana Jeshi la Polisi,” alisema Kibamba.
Akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo, Mkuu wa Idara ya Uchumi Jiji la Mwanza, Jeremia Lubereje, alisema mradi huo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi pamoja na mapato ya ndani ya Jiji la Mwanza.
“Mpaka sasa, mradi umetumia shilingi milioni 152 na umefikia asilimia 90 ya utekelezaji. Gharama za jumla zitakuwa milioni 279, ambapo milioni 237 ni kwa ajili ya vifaa na ujenzi na milioni 41 ni gharama za ufundi,” alisema Lubereje