Dodoma, Agosti 22, 2025
Watumishi wa Tume ya Madini Makao Makuu wamepatiwa mafunzo ya mfumo wa kujisajili katika Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF Self Service), hatua inayolenga kurahisisha mchakato wa usajili wa wanachama na wategemezi wao.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Tume ya Madini, Jacob Mnyenyelwa, jijini Dodoma ambapo amesisitiza umuhimu wa watumishi kuutumia mfumo huo ili kuondokana na changamoto za kiutendaji zinazoweza kujitokeza.
Mnyenyelwa amesema kuwa mfumo wa kujisajili kwa njia ya Self Service ni nyenzo muhimu kwa watumishi na wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya kwani utawezesha usajili kufanyika kwa haraka, uwazi na kwa gharama nafuu bila kulazimika kufika ofisi za NHIF mara kwa mara.
Mafunzo hayo yamefanyika jijini Dodoma na kuendeshwa na wataalam kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).
Washiriki walikuwa ni baadhi ya watumishi wa Idara na Vitengo vya Tume ya Madini walioteuliwa kama Champions, ambao watakuwa na jukumu la kuwafundisha watumishi wengine katika makao makuu ya Tume.
“Mafunzo haya ni muhimu kwa watumishi ambao ni wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya wa Tume ya Madini kwa ajili ya kurahisisha zoezi la kujisajili kwenye mfumo wa NHIF Self Service,” amesema Mnyenyelwa.
Kupitia mfumo huu mpya, wanachama wataweza kujisajili wao binafsi pamoja na wategemezi wao, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuimarisha ushirikiano kati ya NHIF na Tume ya Madini.