Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amewaongoza baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutembelea Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba na Vitalu vya gesi asilia vilivyoko Msimbati Mkoani Mtwara, tarehe 21 Agosti, 2025.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ziara hiyo itawaongezea maarifa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Upekuzi wa Mikataba na utoaji wa Ushauri kwenye Miradi mikubwa ukiwemo mradi huo mkubwa wa gesi na mafuta.
*”Tunapoona mradi huu maana yake ni kwamba kuna mikataba ilitangulia mwanzo mikataba ambayo iliandikwa na kupekuliwa vizuri na vihatarishi vyote vikawekwa vizuri na maslahi ya Taifa yakazingatiwa vizuri.”* Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mafunzo kwa Wataalamu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mafunzo ambayo yatawasaidia kuwaongezea uwezo katika masuala ya kiufundi kuhusiana na miradi mikubwa kama mradi huo wa kuchakata gesi.
*”Kwa kuwa sisi tunafanya kazi hiyo kubwa ya kupekuwa Mikataba na kutoa Ushauri katia Miradi mikubwa kama hii tuliona ni vizuri kwa kushirikiana na TPDC wataalamu wetu wakapata mafunzo ya aina fulani juu ya masuala ya kiufundi ya miradi kama hii.”* Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) Dkt. Eliasi Mwashiuya amesema kuwa ziara hiyo itawasaidia Wataalamu hao kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata mafunzo kwa vitendo kwakuwa mara nyingi wamekuwa wakijadili Mikataba bila kuona changamoto halisi kwenye maeneo husika .
*”Ziara hii itasaidia zaidi mafunzo kwa njia ya Vitendo na kubaini maeneo muhimu ya kutilia mkazo katika kulinda maslahi ya Taifa.”* Amesema Dkt. Elias