Mwenge wa Uhuru umekagua na kuridhia miradi yote 68 yenye thamani ya zaidi ya Sh 26.5 bilioni mkoani Mara.
Miradi hiyo imekaguliwa,kupitiwa na kuwekewa mawe ya msingi kwa muda wa siku tisa baada ya mwenge huo kuwasili mkoani Mara Agosti 15,2025 ukitokea mkoani Simiyu.
Mwenge umehitimisha mbio zake mkoani Mara leo Agosti 23,2025 katika halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini kwa kukagua,kutembelea na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya Sh1.8 bilioni.
Baada ya kumaliza mbio hizo mwenge huo umefika kwenye uwanja wa mkesha katika Shule ya Msingi Kibara ambapo pamoja na shughuli zingine Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Mtelela amesoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati wa usomaji wa risala hiyo mbali uwepo na wakimbiza mwenge kitaifa wakiongozwa na Kiongozi wa Kitaifa wa mbio za mwenge wa uhuru 2025 Ismail Ussi, pia Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi alishiriki kwenye tukio hilo.
Akizungumza katika miradi yote, Ussi alipongeza uongozi wa mkoa wa Mara kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya na halmashauri zote kwa namna ambavyo wameweza kutekeleza miradi mingi yenye tija kwa wananchi.
Amesema usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo uliofanywa na viongozi hao katika miradi hiyo unaleta matumaini kwa wananchi na kuendelea kuwa na imani na Serikali yao.
Ameupongeza uongozi kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kutumia fedha zinazotolewa na Serikali kuu pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri husika.
Ussi alisema miradi yote inalenga kuboresha huduma za kijamii na kutatua changamoto ambazo wananchi walikuwa wakikumbana nazo hapo awali kabla ya uwepo wa miradi hiyo.
Amesema serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi kwa kutekeleza miradi yenye tija ambayo inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Amewataka viongozi wa mkoa huo kuhakikisha miradi ambayo utekelezaji wake unaendelea ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Pia amewataka wananchi kwa pamoja kuhakikisha wanalinda miundombinu ya miradi iliyotekelezwa kwani imegharimu fedha nyingi lakini pia ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha wananchi wengi.
Akizungumza kwenye hitimisho hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi pamoja na mambo mengine amewataka wananchi wote wenyw sifa kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Niwahakikishie wananchi kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki hivyo kila mmoja kwa nafasi yenu hakikisheni mnajitokeza kupiga kura siku hiyo ili kuwachagua viongozi watakaotuleteq maendeleo kwa manufaa na maslahi ya jamii nzima,” amesema Kanali Mtambi
Mwenge wa uhuru utakabidhiwa kesho wilayani Ukerewe mkoani Mwanza tayari kwa kuanza mbio zake mkoani humo.